March 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kakulima:Lushoto ni eneo muhimu kwa shughuli za utalii

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

MAKAMU Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT)Munguabela Kakulima amesema Wilaya ya Lushoto ni eneo zuri kwa masuala ya utalii,hiyo ni kutokana na maeneo yake ya asili ikiwemo misitu, mabonde, milima na hali ya hewa ya baridi.

Ameyasema hayo Machi 21, 2025 wakati anafunga mafunzo ya siku mbili kwa Waongoza Watalii Wilaya ya Lushoto yaliyofanyika kwenye Kituo cha Utalii mjini Lushoto.

Kakulima ambaye ni Makamu Mkuu wa NCT anayesimamia Mipango, Fedha na Utawala, alisema kutokana na umuhimu wa wilaya hiyo kwenye masuala ya utalii, ipo haja kwa waongoza watalii kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwa na weledi katika kuwaongoza watalii.

“Utalii Lushoto ni kutokana na Lushoto yenyewe ilivyo, tayari kwa ukanda wa huku imekuwa kitovu cha utalii.Mfano mimi mwenyewe nimekuwa mtalii,nimefika kwa mara ya kwanza Lushoto jana usiku na nimeona vitu vingi ambavyo sikutegemea kama vipo huku Lushoto, kwanza hali ya hewa yenyewe kutokana na historia ya kuwepo Wajerumani, kumeongeza utalii huo.

“Ili kuendeleza utalii Lushoto, uwezo na umahiri wa kuongoza watalii ni muhimu sana maana wao ndiyo wanaambatana na watalii na kuwaongoza. Na hiyo ni katika kuongeza watalii nchini. Na kwa mwaka huu wa 2025, tulijiwekea lengo la kufikisha watalii milioni tano, hivyo tunachokifanya sisi ni kuona kila mtu anachangia katika kufikisha ile idadi ya watalii ya milioni tano” alisema Kakulima.

Kakulima alisema ili kuufanya utalii kuwa endelevu katika nyanja ya kiuchumi, mazingira na kiutamaduni ni lazima elimu itolewe mara kwa mara hapa Lushoto, na kwa kufuata waliopokea mafunzo haya kuwa kiungo kikubwa kwa ujumla katika utalii, jamii na maendeleo ya utalii hapa Lushoto.

Naye Eunice Ulomi ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo cha NCT, Idara ya Utafiti na Ushauri Shirikishi ambaye pia alitoa mada kwenye mafunzo hayo, alisema wananchi wa Wilaya ya Lushoto wanatakiwa kujivunia kwa kila jambo lililopo Lushoto, na kusema kila kitu kilichopo Lushoto ni Tunu, hivyo kinatakiwa kulindwa na kuenziwa.

Ulomi alisema viongozi wa wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Zephania Sumaye, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge, wamekuwa msaada mkubwa kuendeleza utalii,lakini pia kuwasaidia vijana wa waongoza watalii, jambo ambalo linakuza utalii wilayani humo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt.Mwasyoge,Ofisa Utalii Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Josephat Mwayeya, alisema msukumo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye masuala ya utalii, umechangia wilaya hiyo kuwaendeleza vijana katika kuipenda shughuli ya utalii, hivyo na wao kama halmashauri wamekuwa mstari wa mbele kukuza utalii.

Mwayeya alisema kutokana na umuhimu wa utalii wilayani Lushoto, wamepokea maelekezo, maagizo na ushauri wote uliotolewa na viongozi wa Chuo cha NCT ili kuona wanafanyia maboresho mambo yote yanayogusa shughuli za utalii kwa maendeleo ya wananchi wa Lushoto, wilaya na Taifa.

Akizungumza na mwandishi wa habari katikati ya mafunzo hayo, Katibu wa Waongoza Watalii Wilaya ya Lushoto kupitia Chama cha ULTA, Alphonce Shelukindo, alisema shughuli za utalii kwenye wilaya hiyo imeleta muamko mkibwa kwa vijana kujiunga na shughuli za kuongoza watalii, na wameweza kupata mafanikio makubwa kwa mtu mmoja mmoja, halmashauri na Taifa.

“Shughuli za utalii zimewasaidia vijana kupata ajira. Miaka mitatu iliyopita chama chetu cha waongoza watalii kilianza na vijana 64, na tunaendeleo na shughuli hiyo huku ikitusaidia kupata kipato kizuri na kulea familia zetu. Na tunaushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, umetuwekea Kituo cha Utalii, na sisi ambao tulianza shughuli hii kienyeji, sasa tunaifanya rasmi, na mafanikio yake tumeyaona” alisema Shelukindo.

Katika mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), Chuo cha Taifa cha Utalii, na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, vijana waongoza watalii zaidi ya 40 walipata vyeti vya kuwatambua rasmi katika shughuli zao za utalii.