Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.
MBUNGE wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi ametoa ombi maalamu kwa Shirika la Ndege Tanzania ATCL, akisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa safari mpya za ndege kutoka Arusha, Mwanza na Kigoma hadi Mkoa wa Katavi kwa ajili ya kukuza utalii.
Katika ombi lake, Kapufi amezungumzia jinsi utalii endelevu unavyoweza kubadilisha jamii kugeukia sekta hiyo na kuimarisha uchumi wa maeneo ya ndani ya nchi.
Mbunge huyo, amesema hayo Septemba 28, 2024 akiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambapo kwa kujitolea aliwapeleka wananchi 52 pamoja na wanahabari 8 kwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi jambo ambalo anafanya mara kwa mara kwa makundi mbalimbali.
Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa nchini yenye hazina kubwa ya maliasili kama hifadhi za wanyamapori zinajumuisha Hifadhi ya Taifa ya Katavi na mapori tengefu huku zaidi ya hekari Mil 2.8 zinajumuisha hifadhi za misitu.
Kupitia hazina hizo Kapufi amesema kuna umuhimu wa kuanzisha safari mpya za ndege kwani kunawezekana ipo changamoto watalii wengine kushindwa kufika kutoka pande zote za nchi licha ya kuwepo kwa safari tatu kwa wiki za ndege kutoka Dar es salaam, Tabora na Mpanda.
“Ipo nafasi ya kuanzisha tripu mpya ya ndege ili kutuletea watalii katika maeneo haya hasa kwa wale wanaoona mbali kuja kufanya utalii wa ndani…nitoe rai kwa wazawa kuja kutalii ili kupumzisha akili na kuona uumbaji wa Mungu katika hifadhi hii yenye wanyama wakubwa kama nyati,twiga na viboko ambao ni nembo ya Mkoa wa Katavi” Amesema.
Katika kuendelea kukuza utalii, Kapufi amewaomba wananchi na wanahabari kwa pamoja kushirikiana kutoa hamasa ya utalii kwani utalii unaingiza pato la kigeni kwa nchi na kufungua fursa zingine za elimu,afya na miundombinu ya barabara kujengwa ambapo inategemea fedha kuweza kutekelezwa.
Msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa Katavi Abel Mtui, amesema Hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa ukubwa iko nafasi ya sita kati ya hifadhi 21 nchini na kwa umaarufu yaweza kuwa ya kwanza hivyo inawahitaji wananchi kuitunza na kuihifadhi ili kuondoa changamoto za ukataji miti, uvuvi na uwindaji wa wanyama haramu.
Mtui amesema kwa sasa hifadhi hiyo inapokea watalii zaidi ya 100 kila mwenzi kutoka nje ya nchi hususani mataifa ya Marekani na Uingereza lakini idadi kubwa zaidi ni ya watalii wa ndani.
“Kwa bahati nzuri tuna ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuja kutangaza utalii wetu kupitia Royal Tour ili hifadhi yetu iendelee kupata wageni wengi na wageni wakiwa wengi tunapata ajira na kupata fedha za kigeni” Amesema Mtui.
Ameweka wazi kuwa Royal Tour itaongeza zaidi watalii kwani katika kipindi cha mwezi Julai na Septemba mwaka huu idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 2751.
Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi,Taini Charles amemuomba mhifadhi mkuu kuanzisha mashindano mbalimbali ya michezo ili kuvutia watu wengi zaidi kushiriki katika shughuli za utalii.
Amesema kufanya hivyo watu watajenga moyo wa uzalendo kwa nchi yao na kuongeza ali ya kuanza kuvutiwa kutembelea hifadhi mbalimbali za taifa.
More Stories
Rais Dkt.Samia asajili timu ndani na nje ya Nchi kukabili Marburg
RUWASA Katavi yasaini mkataba ujenzi bwawa la Nsekwa
Wapanda miti 500,kumbukizi ya kuzaliwa Dkt.Samia