March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kafiti  ajitosa rasmi  kuwania Ubunge Ilemela kwa tiketi ya CCM

*Achukua fomu kutoka INEC Agosti 25,2025

*Asindikizwa na  mama yake,viongozi wa CCM na wanaCCM

*Idadi ya wagombea waliochukua fomu yafika 16

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Kafiti William Kafiti,  Agosti 25,2025 amechukua rasmi fomu ya uteuzi wa kugombea Ubunge wa Jimbo  la Ilemela kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Fomu hiyo imetolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kupitia Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ilemela,Herbert Bilia, katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela. 

Kafiti alisindikizwa na viongozi wa CCM Wilaya ya Ilemela, mama yake mzazi, wanachama wa chama hicho, pamoja na wafuasi mbalimbali waliokuja kuonesha mshikamano na uungwaji mkono.

Kwa hatua hii, Kafiti anakuwa miongoni mwa wagombea 16 kutoka vyama mbalimbali vya siasa waliokwisha chukua fomu za uteuzi kwa ajili ya kuwania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Ilemela.

 Vyama hivyo ni pamoja na CCM, CCK, DP, NLD, AAFP, SAU,MAKINI, UMD, N.R.A, ACT, ADA-TADEA, UPDP, UDP, CUF, NCCR-Mageuzi na ADC.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Kafiti William Kafiti,amewaomba wananchi waliomsindikiza kuendelea kushirikiana na kuombeana.

“Nichukue fursa hii kuwashukuru kwa kunisinikiza kuchukua fomu,naomba tuendelee kushirikiana na kuombeana.Agosti 27,2025  itakuwa siku ya kurejesha fomu ya kihistoria,na ndio siku maalum ya historia kwa wanailemela,”amesema Kafiti.