Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
TIMU ya Taifa ya Misri ya mchezo wa Kabaddi inatarajiwa kutua hapa nchini leo mchana tayari kwa mashindano ya Kabaddi ya Afrika ambayo yataanza kutimua vumbi rasmi kuanzia kesho Juni 29 hadi Julai 5, 2021 katika viwanja vya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Katika mashindano hayo ya Afrika nchi zitakazoshiriki ni wenyeji Tanzania, Kenya, Cameroon, Misri, Zimbambwe, Mauritania huku Algeria, Nigeria na Tunisia zenyewe zitatoa wawakilishi wao kuja kushuhudia mashindano hayo kwakuwa timu zao hazitashiriki mashindano hayo.
Kenya italeta timu ya Circle Kabaddi ambayo itachuana na timu ya Magereza kutokana hapa nchini ambapo mchezo huo hautakuwa sehemu ya mashindano bali utachezwa katika mashindano kama sehemu ya onyesho.
Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA), Abdallah Nyoni ameuambia Mtandao huo kuwa, awali timu zote zilitakiwa kuwasili hapa nchini leo lakini walipokea maelekezo ya mabadiliko hivyo kwa mujibu wa ratiba waliyopewa na Shirikisho la mchezo huo la Afrika, na Misri tayari imeshawasili huku Kenya wakitarajiwa kutatua kesho.
Hadi sasa TKSA kwa kushirikiana na serikali kila kitu kinakwenda sawa na kwa upande wa kikosi chao cha timu ya Taifa kilichoweka katika shule ya Sekondari Nguva iliyopo Kigamboni kinaendelea vizuri jambo linalowafanya kutokuwa na wasiwasi wowote kuelekea kwenye mashindano hayo.
Amesema, kwakuwa Tanzania ni mwenyeji basi watahakikisha wanapambana kufa na kupona ili kuweza kufanya vizuri na kuubakiza ubingwa huo hapa nchini jambo litakalosaidia kuitangaza zaidi nchi kimataifa kupitia mchezo huo.
“Tunalishukuru Shirikisho la Kabaddi Afrika kwa kuipa nafasi Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano haya jambo ambalo litachangia kukuza mchezo huu hapa nchini pamoja na kupata fursa ya kuutangaza utalii wetu Kimataifa kwani ni mchezo mkubwa unaotambulika zaidi katika bara la Asia,”.
“Lakini kutokana na Shirikisho la Kabaddi Afrika kutupa heshima kubwa ya kuandaa michuano hii, tutahakikisha tunapambana ili kubakiza kombe hilo hapa nchini jambo ambalo litatupa fursa pia ni kualikwa katika mashindano mbalimbali,” amesema Nyoni.
Kiongozi huyo amesema, hadi walipofikia wamekuwa wakipata msaada mkubwa kutoka kwa washirika wake ambao ni Ofisi ya Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Tanzania, Kamishna Mkuu wa India nchini Tanzania na Patroni wao ambaye amewapa msaada mkubwa hata katika kuiweka kambini timu ya Taifa.
Kutokana na msaada huo mkubwa wanaoupata kuhakikisha wanajiandaa vyema kuelekea kwenye mashindano pamoja na kushiriki kikamilifu ili waweze kunyakuwa ubingwa watahakikisha hawafanyi makosa.
Lakini pia amewataka wadau wa michezo hapa nchini kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo ili kuwapa nguvu vijana wa Tanzania, kuwachangia kwa hali na mali ili waweze kufanikisha mashindano ikiwa wao kama waandaaji, hivyo kama kuna mtu anahitaji kutoa mchango wake afike kambini Kigamboni ambapo timu yao ya Taifa imepiga kambi.
Itakumbukwa kuwa, awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika Desemba mwaka jana lakini yakasogezwa mbele hadi Februari, kisha Aprili ambapo pia yalibadilishwa tena hadi Juni baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Shirikisho la Kabaddi Afrika kilichofanyika Machi, 2021 kupitia Zoom ambacho walikubaliana kubadili tarehe kutokana na masuala ya janga la Corona kuendelea kuzikabili baadhi ya wanachama wake ambao watashiriki katika mashindano hayo.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania