May 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JWTZ yatoa tahadhari dhidi ya matapeli katika nafasi za vijana kuandikishwa Jeshini

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu kuanzia sekondari hadi elimu ya juu, huku likitoa onyo kwa wananchi kuhusu uwezekano wa kujitokeza kwa matapeli watakaojaribu kuwalaghai waombaji.

Akizungumza Leo Aprili 30,2025 katika Makao Makuu ya JWTZ jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Jeshi hilo, Kanali Gaudentius Ilonda, alisema kuwa wapo baadhi ya watu watakaojitokeza na kuwatapeli watu kwamba wanaweza kuwasaidia kupata nafasi hizo Ili wajioatie fedha kwa njia hiyo ya udanganyifu.

“Wananchi msikubali kurubuniwa na matapeli watakaojitokeza kwa madai ya kuwawezesha wqombaji kujiunga na Jeshi kwa malipo ya fedha,

” Hakuna utaratibu wa kupata nafasi hizi kwa kutoa fedha,hii ni rushwa, na yeyote atakayebainika kushiriki katika vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesisitiza Kanali Ilonda.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, uandikishaji huo unahusisha vijana wenye taaluma adimu nchini, ambapo wataalamu hao watapatiwa mafunzo ya kijeshi sambamba na ya kuendeleza taaluma zao.

Amesema  taaluma zinazohitajika ni taaluma ya Tiba ambapo wanahitaji madaktari bingwa binadamu , wahandisi na mafundi mchundo.

Kanali Ilonda amebainisha kuwa waombaji wote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania, wenye vitambulisho vya Taifa, afya njema ya mwili na akili, nidhamu nzuri, na wasiwe na rekodi ya makosa ya jinai.

Sifa nyingine zinazohitajika ni pamoja na kuwa na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya kitaaluma, na wawe hawajawahi kuhudumu katika Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo, wala Kikosi cha Kuzuia Magendo na awe amehitimu Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mkataba wa au mujibibwa Sheria na kutunukiwa cheti kwa wale waliomaliza mkataba wa kujitolea.

Amesema  waombaji wa kidato cha nne na sita wasizidi miaka 24; wenye elimu ya stashahada wasizidi miaka 27; na madaktari bingwa wa binadamu wasiwe na zaidi ya miaka 35.

Kanali Ilonda amesema kuwa maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe katika Makao Makuu ya Jeshi, Dodoma, kuanzia Mei 1 hadi Mei 14 mwaka huu.