March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jumuiya ya Wazazi CCM yahimizwa kuwalea vijana kwa maadili

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, imehimizwa umuhimu wa malezi bora kwa vijana kuwa, ni nyenzo ya msingi ya kutunza maadili, kuhakikisha usalama na maendeleo ya jamii ili kuimarisha ustawi wa taifa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’,ametoa kauli hiyo alipofungua kikao cha kawaida cha Jumuiya hiyo,kilichofanyika jijini hapa, ili kuzungumzia maendeleo na kuchambua changamoto za kijamii na kisiasa zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na wajumbe wa jumuiya hiyo, Smart amesema, Jumuiya ya Wazazi ina kazi ya kuongoza mchakato wa malezi na utunzaji wa vijana, kuhakikisha wanawalea katika maadili mema na kuwa raia wema wenye kuunga mkono misingi ya amani, utulivu na maendeleo endelevu.

“Wazazi ni nguzo muhimu ya jamii. Tunapaswa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili mema ambayo yatakuwa msaada kwao binafsi na kwa taifa kwa ujumla, katika mustakabali wa kujenga kizazi na taifa lenye maadili bora,”amesema Smart.

Amesema kuwa, changamoto zilizojitokeza kwa baadhi ya maeneo Oktoba 29, 2025 zilitokana na ukosefu wa malezi bora na upungufu wa msukumo wa maadili katika familia na jamii, jambo lililochochea vurugu na migogoro isiyokuwa ya lazima.

“Mnayo kazi kubwa ya malezi ya vijana.Yaliyotokea Oktoba 29, 2025, yalitokana na vijana kukengeuka maadili ya Kitanzania, hivyo mna kazi ya kuwalea katika maadili mema kwa maslahi ya chama, jamii na taifa,”amesema.

Sanjari na hayo amesisitiza kuwa Jumuiya ya Wazazi ni moja ya nguzo muhimu za CCM kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, inalenga siyo tu malezi ya vijana bali pia utunzaji wa mazingira, elimu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Jumuiya ya Wazazi, iliyotimiza miaka 48 tangu kuanzishwa kwake 1955, awali ilijulikana kama TAPA, kabla ya kubadilika jina 1978, imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii na kisiasa ndani ya CCM.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mwanza, Mohamed Lukonge, amesema kikao hicho kilipaswa kufanyika Desemba 2025, kilikuwa fursa muhimu ya kujadili nyanja mbalimbali za maendeleo ya jumuiya, malezi, utunzaji wa mazingira na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wajumbe.