Na Esther Macha, Timesmajira Online – Mbeya
JUMUIYA ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Mkoa wa Mbeya, kwa kushirikiana na Kamati za Amani za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, imetoa wito kwa wananchi kuepuka chuki, vurugu na maandamano ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ikisisitiza kuwa amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote.
Tamko hilo limetolewa Oktoba 23, 2025, na Prof. Donald Mwanjoka, Katibu wa JMAT Mkoa wa Mbeya, wakati wa mkutano wa viongozi wa dini kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa uliofanyika kwa lengo la kuliombea Taifa amani kuelekea uchaguzi huo.
“Tumekaa kama viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali tukiwa kama walezi wa jamii. Tunawahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa amani na utulivu, wajitokeze kupiga kura na kufanya maamuzi ya busara ya kuchagua viongozi waadilifu watakaowaongoza,” amesema Prof. Mwanjoka.
Ameongeza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha vurugu, maandamano au migawanyiko katika jamii, akisisitiza kuwa amani ni urithi wa thamani unaopaswa kulindwa daima.
Aidha, Prof. Mwanjoka amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuepuka kauli au matendo yanayoweza kuhatarisha amani, huku akiitaka Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, huru na unaoaminika.
“Katika kipindi hiki tunachoelekea uchaguzi mkuu, tunaendelea kuliombea taifa letu na kusisitiza kulinda amani kwa gharama yoyote, tukitambua athari kubwa zitakazojitokeza endapo amani itatoweka,” ameongeza.
Kwa upande wake, Askofu Jacob Kahemele wa Kanisa la Anglican Jijini Mbeya, amesema kuwa taharuki kuelekea uchaguzi ni jambo la kawaida, akilinganisha mchakato wa uchaguzi na hali ya mama mjamzito anayepitia mabadiliko mbalimbali kabla ya kujifungua.
“Hakuna uchaguzi unaopita bila taharuki. Hizo ni dalili za mabadiliko. Mungu ametuumba kwa mitazamo tofauti, hivyo ni wajibu wetu kama viongozi wa dini kuendelea kujenga amani na umoja,” amesema Askofu Kahemele.
Naye Sheikh Ayas Msafiri Njalambaa, Makamu Mwenyekiti wa JMAT kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa viongozi wa dini katika kipindi cha uchaguzi, akisema kuwa haki ya kupiga kura ni wajibu wa kisheria unaopaswa kufanywa bila kushinikizwa.
“Tudumishe amani na tusiruhusu mtu yeyote kutupokonya utulivu tulioujenga kwa muda mrefu. Dini zote zinafundisha upendo, umoja na heshima,” amesema Sheikh Njalambaa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina