Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online Mwanza
JUMUIYA ya Maridhiano na Amani Tanzania Mkoa wa Mwanza, imewashauri viongozi wa dini ya Kiislamu na taasisi za dini hiyo,kuwa kioo cha kulinda na kutunza amani badala ya kuibua migogoro isiyo na tija.
Ushauri huo ulitolewa jijini hapa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Mwanza,Alhaji Sheikhe Mussa Maulid Kalwanyi alipozungumza na timesmajira online kuhusiana na kudumisha amani na kuepuka migogoro katika jamii.
Amesema migogoro mingi inayoendelea jijini Mwanza imejikita katika maslahi kuliko imani na kumcha Mwenyezi Mungu,ili kuiepuka viongozi wa dini na taasisi za Kiislamu wanatakiwa kuwa kioo cha kulinda na kutunza amani iliyopo na kudumisha utulivu.
Sheikhe Kalwanyi amesema amani ni tunu pekee ya kujivunia nchini, wanapotokea wachache wakataka kuivuruga wakijificha katika kivuli cha imani au dini sharti wakemewe wasiingize maslahi yao binafsi kuivuruga.
“Kisa cha suluhu ya udaybiyyah (Dhul-qa’dah 6H) Mtume S.A.W alipotoka Madina kwenda Makka kufanya Ibada ya Umra Maquresh walimzuia kwa kutambua umuhimu wa amani,alilikubali zuio hilo akarudi Madina (Al-Isabah,Juz.Iv Uk wa 468),”amesema.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Maridhino na Amani Tanzania mkoani hapa ameongeza kuwa kitabu cha Waebrania Sura ya 12:14 – 17, kinasema; “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani kwa watu wote.”
Amesema kutokana na vitabu vya dini (Quran na Biblia) vinaasa kudumisha amani,ni dhahiri amani hiyo ina thamani kubwa kuliko nafasi ya mtu yoyote na kueleza kuwa Jumuiya hiyo inaisaidia serikali kushughulikia na kutatua migororo katika jamii kuhakikisha kunakuwa na utulivu,amani na mshikamano.
Amewaomba viongozi dini na waislamu kuwa na subira inapotokea changamoto ya viashiria vya kuvurugika amani katika maeneo yao watafute ushauri,waheshimu na wafuate sheria za nchi.
“Hivi karibuni kulitokea kadhia katika Msikiti wa Masjid Noor-Uhuru,serikali inayoongozwa na Rais Dk.Sami Suluhu Hassan iko makini,itampa haki anayesthili kupewa haki hiyo na kunapokuwa na maelekezo ya serikali wayafuate,kufanya hivyo ni kuheshimu utawala wa sheria,”amesema Sheikhe Kalwanywi.
Pia, amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana,Vignia Sodoka kwa kazi nzuri ya ulinzi wa raia na mali zao kwa kuhakikisha utulivu, usalama na amani vinadumishwa katika jamii wilayani humu.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote