Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) wametoa wito kwa serikali kuachana na mpango wa kutoa elimu ya Katiba ya mwaka 1977 kwa miaka mitatu badala yake kupeleka Miswada ya sheria za mchakato wa katiba Bungeni kwa ajili ya marekebisho.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa JUKATA , Bob Chacha Wakati akizungumza na waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam juu ya Mapendekezo ya JUKATA kuhusu sheria za mchakato wa katiba mpya.
“JUKATA bado tunaamini kuwa hatua iliyotangazwa na wizara ya Katiba na sheria hivi karibuni ya kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu ni hatua ambayo inapaswa kuangaliwa upya kwani tunaamini ni ucheleweshwaji wa kuanzisha mchakato wa katiba”
Aidha JUKATA wametoa wito kwa serikali kuona umuhimu wa kutumia nyaraka muhimu za mchakato wa katiba katika kutunga au kurekebisha sheria za mchakato wa katiba kwani zimezingatia mahitaji ya sasa ya nchi pamoja na uzoefu wa mchakato uliokwama mwaka 2014.
Kadhalika JUKATA wamemuomba Waziri Pindi chana kutoa ratiba ya hatua za mchakato wa katiba mpya ili kuondoa sintofahamu ambayo imetawala miongoni mwa wadau wa katiba na watanzania kwa ujumla.
“Ujio wa Balozi Dkt. Pindi Chana katika Wizara ya Katiba na Sheria tunaamini utaleta Nuru ya upatikanaji wa katiba na kuondoa vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine vinaweza kutukwamisha kama hilo la kutoa elimu ya Katiba ya 1977 kwa miaka mitatu”
Mbali na hayo JUKATA wametangaza sheria mbili za mfano ikiwemo sheria ya marekebisho ya ya Katiba na sheria mfano ya kura maoni pamoja na nyaraka zinazotoa ufafanunuzi juu ya sifa za upatikanaji wa Kamati ya wataalamu pamoja na namna Bora ya usimamizi lakini pia utatuzi wa migogoro inayoweza kutokea katika hatua za mchakato wa katiba mpya.
“Sheria mfano ya mchakato wa Katiba imetoa hatua za mchakato, upatikanaji wa Kamati ya wataalamu, majukumu yake n.k, pia imeainisha namna migogoro inavyoweza kutatuliwa na kusimamiwa katikati ya mchakato” . Amesema Chacha na kuongeza kuwa
“Sheria hiyo imependekeza masuala ya kibajeti na vitu gani vinaweza kufanyika katika hatua za mpito wa nchi kupata katiba mpya”
Kwa upande wake mjumbe wa jukwa hilo, Deus Kibamba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuondoa Dkt. Damas Ndumbaro kwenye Wizara ya Katiba na sheria kwani wanaamini aliona haja ya kutafuta mtu mwingine kwa ajili ya kumsaidia kupitia Wizara hiyo.
Aidha amempongeza Balozi Dkt. Pindi Chana kwa kuwa Waziri wa Katiba na sheria na kumuahidi kumpa ushirikiano katika majumuku yake mapya.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua