Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline, Kilwa
TANZANIA ni kati ya nchi chache duniani ambazo zimejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za asili.
Hata hivyo, raslimali hizo nyingi zilikuwa hazijatumika kikamilifu kuinua uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.
Tatizo lilichangiwa na mambo mengi, lakini kubwa viongozi wetu walikosa maono ya kutumia fursa hizo kikamilifu kuinua wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, tangu Rais Samia Suluhu Hassan, aingie madarakani juhudi zake za kuhakikisha raslimali ambazo hazijawanufaisha Watanzania kikamilifu zinakuwa na manufaa kwao na Taifa kwa ujumla.
Mfano, miongoni mwa rasilimali ambazo zilikuwa hazijanufaisha Watanzania kikamilifu ni eneo kubwa la maji katika Bahari.
Takwimu zinaonesha kuwa nchi yetu imejaliwa maeneo mengi ya maji, ambayo ni muhimu katika shughuli za uvuvi, ambazo huwapatia wananchi lishe, kipato na ajira.
Kwa mfano katika eneo la bahari, Tanzania ina ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilometa 1,424 ambao umegawanyika katika eneo la Maji ya Kitaifa (Territorial Sea) lenye ukubwa wa kilometa za mraba 64,000 na eneo la Ukanda wa Uchumi wa Bahari lenye ukubwa wa kilometa za mraba 223,000.
Lakini takwimu za Wizara ya Mifugo zinaonesha zaidi ya watu milioni nne ndiyo waliendelea kunufaika na sekta ya uvuvi, ikiwamo uchakataji wa samaki, utengenezaji wa zana na vyombo vya uvuvi, biashara ndogo ndogo na mama lishe.
Kwa kutambua umuhimu wa raslimali ya maji katika Bahari, Septemba 19, mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan, aliandika historia mpya katika sekta ya uvuvi baada ya kuweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambayo haijawahi kuwepo tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru.
Kukamilika kwa bandari hiyo kutawezesha meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Pia, uwepo wa bandari ya uvuvi utachochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi.
Hivyo, uwekezaji huu, unaenda kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi kutoka tani 40,721.53 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 249.54 hadi tani 52,937.99 na kuchangia takriban asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2036.
Aidha, Bandari hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira kwa Watanzania takriban 30,000, huku katika hatua za awali za ujenzi, jumla ya ajira za muda mfupi 278 zikiwa zimetolewa.
Kati ya hizo, ajira 106 sawa na asilimia 38 zimetolewa kwa wakazi wa wilaya za Mkoa wa Lindi.
Pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Uvuvi, Rais Samia pia aligawa boti 34 kati ya boti 160 ambazo zinatolewa nchi nzima. Boti hizi kwa ukanda wa bahari ya Hindi zipo 92 zikihusisha wavuvi na wakulima wa mwani.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Rais Samia alisema; “Serikali imejipanga kuhakikisha mazingira ya wavuvi na wakuzaji viumbe maji yanaimarika ndio maana anagawa boti za kisasa zikiwa na kifaa cha kuonesha upatikanaji wa samaki na uhifadhi wa samaki,” anasema Dkt. Samia
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, anashukuru Rais Samia kwa kuamua kutekeleza ujenzi wa mradi huo ambao utakuwa na tija kwa wananchi wa Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Ulega anasema ujenzi huo wa bandari ambao unagharimu sh. Bilioni 280 unakwenda kujibu changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi, lakini pia kuleta fursa za ajira zisizopungua 30,000 kutoka milioni 4.
Aidha, ujenzi huu utawezesha ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki, karakana ya kutengeneza meli, sehemu ya kuhifadhi samaki na uzalishaji wa barafu.
Kwa mujibu wa Ulega, bandari hiyo inakwenda kuongeza ukuaji wa uchumi na Serikali inakusudia sekta ya uvuvi ichangie kwenye pato la taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2026.
“Itawezekana kwa kuwavuta wawekezaji kuja kufunga gati Kilwa Masoko,” anasema na kusisitiza kwamba jumla ya gharama za mradi huo, ni jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya Rais Samia ya kwenda kuinua sekta ya uvuvi nchini na kuhakikisha inakuwa na mchango kwa maendeleo ya taifa.
Mradi huo pia unaungwa mkono na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Uwekezaji kwa kuielekeza Wizara ya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa bandari ya Uvuvi inayojengwa Wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.
Akizungumza na waandishi wa habari Menyekiti wa Kamati hiyo, David Kihenzile , Mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini anasema uamuzi huo wa Serikali ni kwa ajili ya kuongeza Kasi ya uvunaji wa mazao ya bahari na kusaidia ukuaji wa uchumi.
Naye mvuvi Abdallah Ally, anashukuru Rais Samia kwa kuwapatia mkopo wa boti wenye gharama nafuu, akisema boti hizo zitawasaidia kwenye shughuli zao.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa bandari hiyo, Ally, anasema utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi nchini, kwa kuwa utaongeza mazao ya samaki yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja na ujenzi wa viwanda.
Aidha, anasema mradi huo utakuwa kichocheo cha uchumi, itaongeza ajira na upatikanaji wa samaki wa kuboresha.
Akizungumza kwa simu mmoja wa wafanyabiashara, Paul Swai, ambaye alihudhuria hafla ya utoaji tuzo kwa wenye viwanda waliofanya vizuri iitwayo President Manufacturer of the Year (PMAYA), ambazo huandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), anasema mradi wa bandari ya uvuvi utakuwa na tija kwa taifa.
“Wote tumemsikia Rais Samia, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara hali ambayo imewavutia wafanyabiashara na wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.
Kwa sasa hakuna mtu anayedaiwa kodi kwa mtutu wa bunduki, kwa hiyo tutegemee mradi huu wa bandari ya Kilwa utazalishaji viwanda vingi vya samaki.”
Swai anasema dhamira ya Serikali ni kuwashwa mtambo mmoja kuanza kuzalisha umeme na katika Bwawa la Mwalimu Nyerere Januari, mwakani lazima iendane na kasi ya ujenzi wa viwanda vitakavyotumia umeme huo, vikiwemo vya samaki.
Akimnukuu Rais Samia, Swai anasema; “Aprili utawashwa mtambo mwingine hali itakayosaidia kupatikana umeme wa kutosha na kuondoa malalamiko ya uhaba wa nishati hiyo.
Kwa hiyo umeme huo utaapowashwa kupitia Mradi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa, viwanda vingi vya samaki viwe vimejengwa, kwa hiyo navyo vitanufaika na umeme huo.”
Anasema utajiri wa rasilimali za uvuvi nchini utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na sekta ya viwanda.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani