November 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Juhudi za pamoja zahitajika kutokomeza Malaria na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele 2030

Na.WAF-Kigali

Juhudi za pamoja na Ubunifu baina ya Serikali na Sekta mtambuka zinahitajika ili kutokomeza Ugonjwa wa Malaria na Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Beatrice Mutayoba akimuwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwenye Mkutano uliolenga kujadili kuhusu Ugonjwa wa Malaria na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele uliofanyika Jijini Kigali, Rwanda.

Akiwasilisha mada kwa niaba ya Waziri Ummy iliyojikita kwenye kutumia ubunifu mbalimbali katika kuharakisha kufikia malengo yaliyowekwa katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo Barani Afrika, yaani kuyatokomeza kabla au ifikapo mwaka 2030, Dkt. Mutayoba amesisitiza umuhimu wa kujumuisha sekta mtambuka katika kukabiliana na magonjwa haya badala ya kuiachia Sekta ya Afya pekee.

Dkt. Mutayoba ameelezea namna Tanzania inavyotumia ubunifu katika utekelezaji wa afua mbalimbali za Malaria na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele katika kuharakisha kufikiwa lengo la kutokomeza magonjwa hayo nchini Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.

“Kwa upande wa Malaria, tumegawa nchi kulingana na ukubwa wa ugonjwa ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi ikiwa pamoja na kuhusisha wadau nje ya sekta ya afya, kama Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Madiwani kutumia kadi za alama (scorecards), utoaji wa kingatiba za kudhibiti ugonjwa wa Trakoma mara mbili kwa mwaka badala ya kutumia dawa mara moja kama ilivyokuwa hapo awali” amefafanua Dkt. Mutayoba.

Ubunifu mwingine alioueleza ni pamoja na uanzishwaji wa Baraza la Kutokomeza Malaria ili kusaidia upatikanaji wa rasilimali za kupambana na Malaria kwa kuhusisha sekta mtambuka.

“Ili kuweza kudhibiti mbu waenezao Malaria ambao wameanza kujenga usugu dhidi ya dawa zinazotumika kwenye vyandarua kwa sasa, Wizara imeanza kutekeleza maelekezo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kuanza hatua za awali za majadiliano za kuzalisha vyandarua vya kisasa nchini Tanzania kwa kushirikiana na Sekta Binafsi ili kutatua tatizo la usugu wa mbu waenezao Malaria” .

Hata hivyo Dkt. Beatrice amewataka washiriki wa kilele hicho kuunga mkono jitihada za matumizi ya ubunifu ili kwa pamoja kuweza kufikia lengo la kutokomeza Malaria na Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ifikapo 2030.