October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa Kagera. Brigedia Jenerali Marco Gaguti akikabidhi jezi kwa moja ya timu kabla ya kuanza mashindano ya JPM BODA BODA CUP 2020.

JPM Bodaboda Cup 2020 yaanza rasmi Kagera, washindi kuzawadiwa mamilioni

Na Allawi Kaboyo, Bukoba

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amezindua mashindano ya mpira wa miguu ambayo yatawashirikisha waendesha pikipiki maarufu bodaboda yatakayozijumuisha timu 18 kutoka halmashauri sita za mkoa huo.

Gaguti ameeleza lengo la mashindano hayo kuwa ni kuwaweka vijana hao pamoja na kuwapa elimu juu ya ujasiriamali, elimu ya usalama barabarani pamoja na elimu ya ulinzi na usalama ili vijana kwa wingi wao waweze kushiriki katika suala zima la kutunza amani, kwani wanakutana na wananchi mbalimbali wenye taarifa nyingi.

Ameongeza kuwa, vija wa bodaboda ni muhimu sana kwenye jamii hasa kwenye usafirishaji, lakini pia katika suala zima la kulinda amani maana hutumika pia baadhi yao kuwasafirisha wahalifu.



Baadhi ya waendesha pikipiki maarufu BODA BODA wakiwa kwenye maandamano ya kuashiria kuanza rasmi kwa mashindano ya JPM BODA BODA CUP 2020 mkoani Kagera.

“Tumeweka mashindano haya mahususi kabisa ili kuwafanya vijana kuwa pamoja ili kuweza kuwajengea uwezo wa ujasiriamali maana kazi hii ya usafirishaji ina mwisho wake, lakini mtu akiwezeshwa katika njia nyingine ataweza pia kujiendeleza kimaisha na kiuchumi,”amesema RC Gaguti.

Mashindano hayo yanazihusisha kata 14 za Manispaa ya Bukoba na timu nyingine kutoka halmashauri ya wilaya Muleba, Karagwe, Missenyi na halmashauri ya wilaya Bukoba na mchezo wa ufunguzi umezikutanisha timu za kata ya Kashai na Bilele.



Mkuu wa Mkoa Kagera Brig. Jen. Marco Gaguti akikagua timu kabla ya mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya JPM BODA BODA CUP 2020 katika uwanja wa shule ya msingi Kashai Manispaa ya Bukoba.

Aidha, amesema kuwa nje mchezo wa mpira wa miguu yatahusisha mashindano ya vipaji ya uimbaji kwa wasanii wa mkoa huu ambapo nao pia watapata zawadi zao.

Mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atapa kitita cha shilingi milioni 3.5, mshindi wa pili shilingi milioni 2.5 na mshindi wa tatu shilingi milioni 2.