January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Joshua Nassari

Joshua Nassari ajiunga CCM, aibua maswali, atakiwa kuomba radhi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha

ALIYEKUWA Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Joshua Nassari, ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM.

Nassari ambaye alivuliwa ubunge wa jimbo hilo kwa kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila kutoa taarifa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametangaza uamuzi huo leo kwenye ofisi za CCM mkoa wa Arusha.

Hafla ya kumpokea Nassari ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM mkoa wa Arusha.

Amesema amekuwa mbunge akiwa mdogo kuliko wote Tanzani na kama ni kazi aliwafanyia watu wake wa Arumeru Mashariki. Amesema alipoingia kwenye siasa akiwa mdogo sio kwamba alikuwa haioni CCM, bali ilikuwa bado hajaamua kufanya hivyo.

Sababu za kujiunga CCM

Amesema hajatangaza nia mahali popote kwamba anajiunga na CCM kwa ajili ya kutangaza nia ili kugombea nafasi yoyoye. Kwa mujibu wa Nassari haikuwa kazi rahisi kufanya maamuzi ya kuhama CHADEMA na kujiunga CCM.

“Leo nimekuja kwenu rasmi mchana kweupe kwa sababu ninachokifanya leo ni suala ambalo liko wazi na lenye mwanga wa kumwelekeza,” amesema Nassari na kushangiliwa na wana-CCM.

Amesema amekuja mbele ya wana-CCM kwa sababu anaipenda nchi yake (Tanzania), kwani angekubali kukaa duniani (nje ya nchi) atunze familia yake akiwa huko na asome magazeti ya Tanzania akiwa huko, lakini ameona asifanye hivyo, kwani anawaza kizazi cha jamii yake.

Akabidi kadi ya CHADEMA

Nassari katika barua yake ya kuomba kujiunga na CCM ameambatanisha kadi ya chama chake cha zamani (CHADEMA). Nassari wakati akiwa mbunge CHADEMA pamoja na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alikuwa mstari wa mbele kuwashtumu wabunge wa Chama hicho waliokuwa wakijiunga na CCM akiwatuhumu kununuliwa.

Tuhuma za madiwani CCM kununuliwa

Wakati akiwa CHADEMA, Nassari aliwahi kusema wabunge na madiwani wa chama hicho wanaojiunga na CCM kwa kutangaza kuunga mkono juhudi za Serikali wananunuliwa.

Nassari alidai ana ushahidi wa suala hilo ambapo kwenye mkutano mmoja na waandishi wa habari uliofanyika Arusha alionesha kile alichoita ushahidi wa video akidai inaonesha jinsi baadhi ya madiwani wao wanavyoshawishiwa na viongozi wa Serikali kukihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Kabla ya kufanya hivyo, Nassari na Lema, walikuwa wameahidi waandishi wa habari kwamba wangeanika ushahidi huo hadharani ili kuonesha mbinu walizoziita chafu, zilizofanywa na viongozi wa Serikali kwa madiwani wao.

Ushahidi aliokuwa akiutumia

Katika hicho alichokiita ushahidi huo, walionekana madiwani waliokuwa wa chama hicho kwa nyakati tofauti wakizungumza na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti na viongozi wengine.

Alidai mazungumzo kati ya viongozi hao wa Serikali na madiwani hao, yalihusu kuhama kwa madiwani hao na ahadi walizotakiwa kupewa baada ya kutimiza nia hiyo.

Katika video ya kwanza iliyochukua dakika zipatazo 30 baada ya kurekodiwa Agosti 28, mwaka huu, alionekana mtu mmoja akionekana akizungumza na mmoja wa madiwani wa Chadema akidai alikuwa akimshawishi ahamie CCM. Nassari alisema vifaa alivyotumia kunasa mazungumzo ya madiwani hao alitoka navyo Ulaiya alipokuwa masomoni, ambapo baadaye aliwasilisha ushahidi wa CD hizo kwa TAKUKURU.

Aibua maswali magumu

Kujiunga kwa Nassari CCM kumeibua maswali mazito kwa wachambuzi wa masuala ya siasa yakihoji sababu za yeye kuwatuhumu madiwani na wabunge waliokuwa wakinga mkono juhudi za Serikali baada ya kuona kile walichokuwa wakikipigania wakiwa upinzani, ndicho hicho kilifanywa na Serikali ya CCM.

Atakiwa kuomba radhi

“Wenzake waliokuwa wakiona kazi nzuri iliyofanywa na Serikali alikuwa akidai wananunuliwa, leo hii naye amekuja huku kwetu, kabla ya kukubaliwa kujiunga na CCM alitakiwa atoke mbele kwa waandishi wa habari aonbe radhi Chama na aseme zile CD alizokuwa akizunguka nazo zilikuwa za kupika,” amesema mmoja wa makada wa CCM.