Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo amewataka wananchi wa Korogwe na Watanzania wote kuwa na imani na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala la uwekezaji kwenye bandari ya Dar-es -Salaam.
Jokate amesema wanaopinga suala hilo hawataki mafanikio ya serikali ya awamu ya sita iliyo chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani kufanikiwa kwa Serikali hiyo, ni anguko kwao, na kuanguka kwa Serikali hiyo ni mafanikio kwao.
Ameyasema hayo Julai 18, 2023 kwenye mkutano wake na vyombo vya habari q kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe ambao ni utangulizi wa mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo utakaofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Mazoezi mjini Korogwe Julai 19, 2023.
“Jambo hili la uwekezaji kwenye bandari zetu ni jambo jema na Watanzania wanatakiwa waendelee kuliunga mkono, kuna watu wameona wameshikwa pabaya ndiyo maana wanalipinga,likifanikiwa ni mafanikio kwa CCM na mafanikio ya serikali,”ameeleza Joketi na kuongeza kuwa
“Rais Dkt. Samia ni mama hakuna mama au mwanamke yeyote mwenye akili timamu anaeweza kutelekeza watoto wake,tunaamini kwa makubaliano haya ya kuendeleza bandari zetu hawezi kutuingiza chaka,”.
Mwegelo amesema Rais hakukurupuka kwenye jambo hilo, Juni 10, mwaka huu alilipeleka bungeni na wabunge wakaridhia mchakato uendelee, lakini pia likaenda kwenye vikao vya juu vya CCM, nao wakakubali kuwa lina manufaa kwa taifa.
“Jambo hili Rais Dkt. Samia hakulifanya kimya kimya, bali alilipeleka bungeni, na wabunge wakaridhia mchakato uendelee, lakini pia likaenda kwenye vikao vya juu vya CCM, nao wakakubali kuwa lina manufaa kwa taifa,”.
Mwegelo amesema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali za kutosha, lakini wameendelea na nadharia badala ya kuziendeleza,ndiyo maana hatujapiga hatua za kutosha moja ya rasilimali hizo ni bandari ikiwemo ya Dar-es-Salaam ambayo inategemewa na nchi karibu nane (8) hasa zilizo kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu.
Hivyo ni lazima wakafanya maboresho makubwa kwenye bandari ya Dar-es-Salaam ikiwemo mitambo, teknolojia na miundombinu ya kisasa.
Na ili kufanikisha hilo, ni lazima apatikane mwekezaji wa uhakika na mwenye nguvu na mtandao mkubwa wa biashara na uzoefu wa kwenye mataifa mengine, na mtu huyo ni DP World ya nchini Dubai.
Mwegelo amesema kikubwa wananchi waendelee kupewa elimu juu ya jambo hilo la uwekezaji kwenye bandari zetu na kuongeza kuwa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Chongolo itakayofanyika Julai 19, 2023 mjini Korogwe, itamaliza kazi na wananchi wataelewa zaidi umuhimu wa uwekezaji huo, kwani ataongozana na wataalamu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando amesema wanaitetea serikali kwa kila jambo jema inalofanya kwa ajili ya maslahi ya wananchi na taifa inapotokea upotoshaji, basi ni haki yao kusema mustakabali wa nchi na kuzungumza yaliyoahidiwa na serikali.
“Nakupongeza Jokate kwa kuandaa jambo hili linaloweka sawa jambo la kesho wananchi waelewe kuna wataalamu watazungumza katika kuelezea jambo hilo ukweli ni kwamba, wapo watu wamebobea kwenye masuala haya ya uchumi na kueleza faida za uwekezaji kwenye bandari zetu. Hivyo wakishazungumza wao, na wewe mwananchi sasa ndiyo utazungumza, maana utakuwa na uelewa kuhusu jambo hilo,”amesema Msando.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga James Kaji,amesema ana fahamu umuhimu wa bandari sababu ni lango kuu la biashara ili kuleta ufanisi ni vizuri yakafanyika maboresho katika uwekezaji na usimamizi mzuri wenye kukidhi viwango vya kimataifa katika kutoa huduma.
Kwa takribani miezi miwili sasa, kumekuwa na mjadala mzito nchini kuhusu Mkataba wa Makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi ya Tanzania na Dubai baadhi wakisema mkataba huo utakuwa chachu ya kuendeleza bandari zetu na kupata mafanikio makubwa tangu nchi kupata uhuru lakini wengine wakipinga makubaliano hayo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba