November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jokate: maji yamefika Mji wa Korogwe, kupatikana kwa asilimia 87.8

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji Mashindei, na kusema adhima ya kuwapatia maji safi wakazi wa Mji wa Korogwe inakwenda vizuri.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza (wa pili kulia). Ni baada ya kufika kwenye chanzo cha maji Mradi wa Maji Mashindei, kilichopo Kijiji cha Mashindei, Kata ya Lewa, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Kulia ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji, CPA Joyce Msiru.

Ni baada ya kutembelea mradi huo Julai 12,2023ambao Serikali imetoa kiasi cha bilioni 1.6 ili kuona chanzo kipya cha maji kinajengwa kutoka Kijiji cha Mashindei kilomita 12 kutoka Mji wa Korogwe, na ukarabati mkubwa unafanyika kwa kuweka mabomba mapya ya usambazaji maji kwenye Mji wa Korogwe pamoja na mradi wa visima virefu saba.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye Mtaa wa Mtonga mara baada ya kumaliza ziara hiyo iliyoanzia kwenye chanzo cha maji Kijiji cha Mashindei na kumalizia kwenye moja ya matenki yatakayopokea maji hayo lililojengwa kwenye Mtaa wa Kwamkole, Mwegelo amesema dhamira ya serikali ni ya dhati kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Chanzo cha maji Mradi wa Maji Mashindei unaopeleka maji katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga.

“Waziri wa Maji Jumaa Aweso, aliagiza na kutoa miezi mitatu maji yawe yamefika kwenye Mji wa Korogwe na kweli wataalamu wetu wa maji wakiongozwa na Mhandisi Mgaza tumewaona wamefanya kazi kubwa usiku na mchana na maji yamefika Mji wa Korogwe sasa wananchi wanatumia maji masaa 24, hasa hapa Kata ya Mtonga,”amesema Mwengelo.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo akipanda kwenye tenki la maji lililopo Mtaa wa Kwamkole, Kata ya Mtonga. Tenki hilo lenye ujazo wa lita 225,000 ni moja ya matenki yanayopokea maji kutoka mradi wa maji Mashindei kabla ya kusambazwa kwenye Mji wa Korogwe.

Ameeleza kuwa wananchi walikuwa wanapata maji kwa asilimia 32 na sasa wanapata kwa asilimia 87, hii ni dhamira njema ya Serikali na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuondoa kero ya maji.

“Ninachoomba kwenu, nataka mtunze mazingira ili nayo yatutunze leo hii nimetoka Mashindei kilipo chanzo cha maji kule mvua inanyesha lakini huku hakuna mvua, hivyo wenzetu kule wametunza mazingira ndiyo maana sisi huku tunapata maji sasa na sisi tutunze mazingira,”amesema Mwegelo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza ambaye anasimamia utoaji huduma kwa muda kwenye
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mji wa Korogwe (KUWASA), amesema mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji kwenye Mji wa Korogwe.

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji, CPA Joyce Msiru akipanda kwenye tenki la maji lililopo Mtaa wa Kwamkole, Kata ya Mtonga lenye ujazo wa lita 225,000 ni moja ya matenki yanayopokea maji kutoka mradi wa maji Mashindei kabla ya kusambazwa kwenye Mji wa Korogwe.

Mhandisi Mgaza amesema mradi wa maji Mashindei kwa kushirikiana na vyanzo vingine vya maji ikiwemo mradi wa visima virefu saba katika Mji wa Korogwe utaondoa kabisa shida ya maji katika mji huo, huku akibainisha kuwa Kata zote 11 zilizopo kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe zitapata maji ya bomba.

Mgaza amesema kazi ya kuweka mabomba mapya ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 24 kwenye Mji wa Korogwe zinaendelea ili kuona maji hayo yanawafikia wananchi wote wa Korogwe kwa muda uliopangwa.

Huku maji yatakayozalishwa na vyanzo vyote vya maji kwenye Mji wa Korogwe ni lita za ujazo milioni 5,523,000 kwa siku sawa na asilimia 87.8, wakati mahitaji ya wakazi ni lita milioni 6,286,000 kwa siku.

“Baada ya chanzo cha mradi wa maji Mashindei kukamilika na kuweza kufikisha maji kwenye Mji wa Korogwe kwa mabomba yenye urefu wa kilomita 12, wananchi watapata maji kwa asilimia 87.8. Kinachofanyika sasa ni kuwekwa miundombinu mipya ya bomba kuu la usambazaji maji lenye urefu wa kilomita 24 katika Mji wa Korogwe,”amesema Mgaza.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya ziara ya kukagua mradi wa maji Mashindei.

Naye, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji, CPA Joyce Msiru ameshukuru uongozi wa Wilaya ya Korogwe ukiongozwa na Mwegelo kwa kuwapa ushirikiano hadi kufikia hatua hiyo, huku akiwataka wananchi kulipia maji hayo ili miradi ya maji iwe endelevu.

Nao wananchi wa Mtaa wa Mtonga Kati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walikiri kupata maji kwa sasa, ambapo Veronika Bakari amesema kwa sasa wanapata maji ya bomba, huku Jenifa Hussein akisema pia wanapata maji hayo, lakini kwa wiki mara tatu mpaka nne.