Na David John, TimesMajira Online
WAKATI Watanzania wakisherehekea Siku ya Uhuru, ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo Desemba 9, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate Mwegelo ameitumia siku hiyo kushiriki kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Janguo, Mloganzila pamoja na ujenzi wa mradi mkubwa wa shule ya Sekondari ya Wilaya ya Kisarawe ambao utagharimu Sh.milioni 700.
Katika hatua ya kukagua na kushiriki ujenzi wa madarasa hayo, Jokate aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mussa Gama ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kutaka halmashauri zote nchini kujenga vyumba vya madarasa ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba 2020 wanajiunga na masomo ya kidato cha kwanza ifikapo Januari 2021.
Akizungumzia hilo Jokate amesema, wameamua kuitumia siku hiyo ambayo Watanzania wanaadhimisha miaka 59 tangu kupata Uhuru wake, kwa kuangalia eneo la sekta ya elimu na hasa katika kutatua changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo mwaka huu Kisawe waliofauli wanafunzi 2488.
Hata hivyo, wameweka mikakati kuhakikisha wanafunzi wote waliofauli katika Wilaya ya Kisarawe ifikapo Januari mwakani shule zinapofunguliwa wakute vyumba vya madarasa vipo tayari.
Akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa Sekondari ya Kisarawe ambayo itagharimu kiasi cha Sh. milioni 700, Jokate amesema, kimsingi ujenzi wa Sekondari hiyo unakwenda kuondoa changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu wa kwenda na kurudi shuleni.
“Kata hii ya Kazimzumbwi ilikuwa na chagamoto ambapo ya shule ya Sekondari, ukipita barabarani unakutana na wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.Umbali umesababisha wanafunzi wanaingia darasani saa tatu asubuhi na huwezi kuwahukumu kutokana na hali halisi ya umbali uliyopo wa kufika shule.
“Kwa wa wakazi wa Kazimzumbwi ninafuraha nyingi sana kupata mradi huu wa ujenzi wa Shule ya Sekondari wenye thamani ya Shilingi milioni 700 na shule hii ndio inabeba jina la Wilaya ya Kisarawe, shule hii itakuwa na madarasa nane, matundu ya vyoo, Maabara, Bwalo, Nyumba za walimu na ofisi.
“Kwa kweli tunakwenda kujenga shule ambayo itatoa taaswira mpya ya mji wa Kisarawe na hii inatokana na juhudi za Mbunge wetu Selemani Jafo ambaye ameapishwa tena na amesema, anakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya kuelekeza katika shule hiyo ambayo itakuwa ya mfano katika wilaya ya Kisarawe,” amesema Jokate.
Jokate ameongeza, mafanikio ya mradi huo yapo kwenye mikono ya wananchi na iwapo mradi utakwama nao utakuwa umekwamishwa na wananchi.
Amewaomba wananchi kuwa walinzi kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinakuwa salama na hakuna sababu ya wananchi kuutia dosari mradi huo wa ujenzi wa sekondari ya Kisarawe na kwamba ujenzi wa sekondari hiyo ni muhimu ambao utakuwa na jengo la ghorofa.
Kwa upande wake Msimamizi wa ujenzi wa Sekondari hiyo kutoka Jeshi la Polisi Herman Mayala amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwamba ujenzi wa sekondari hiyo utakamilika kwa wakati na wanafunzi wataingia shuleni kama ratiba ya kufungua shule inavyooleza.
“Ndio maana tumepiga kambi hapa kuhakikisha tunajenga usiku na mchana , hatutalala, tutafanya ujenzi wakati wote. Nakuhakikishia Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, ujenzi wa shule utakamilika kwa wakati na wanafunzi wataanza masomo yao kama kawaida. Tumejipanga na tuko tayari kuifanya kazi hii kwa ubora mkubwa,”amesema Mayala.
Mbali na hivyo, pia Jokate ameshiriki kwa hatua ya awali ujenzi wa madarasa mawili katika Sekondari ya Jenguo iliyopo Kata ya Msanga ikiwa ni kuanza kutekeleza kwa kauli ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa. Huku akisema
halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ina upungufu wa madarasa saba na kati ya hayo madarasa mawili ni kutoka Shule ya Sekondari Janguo, hivyo amewapongeza wananchi na Mwalimu Mkuu kwa uamuzi wao wa kuanzisha ujenzi wa vyumba hivyo.
“Nimefurahishwa na wananchi kwa jinsi ambavyo wameona umuhimu wa elimu kuhakikisha wanatoa fedha Sh. milioni tano wa ajili ya kuanza ujenzi, nami kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya nitachangia Sh. milioni 15. Nataka madarasa haya hadi inapofikia Desemba 30 mwaka huu yawe yamekamilika na ifikapo Januari 2021 watoto waingie darasani kusoma. Shule zitafunguliwa Januari 11, 2021,”amesema.
Ameongeza kwamba kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali kupitia Waziri Mkuu, hakuna likizo hivyo Kisarawe wameona watumie siku hii ya 9 Desemba kushiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kutoa fursa kwa watoto kupata nafasi ya kujiunga na msomo katika muhula mpya wa masomo.
Aidha amepongeza juhudi za wananchi wa Kata ya Msanga kwa kuona umuhimu wa madarasa kwani kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe Mussa Gama, kuanzia mwaka wa masomo 2018 kulikuwa na ongezeko la wanafunzi 145, mwaka 2019 wanafunzi 150 na mwaka 2020 lilikuwa 219 na mwaka huu kuelekea 2021 ongezeko ni wanafunzi 190, hivyo nawapongeza wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Wakati huo huo akiwa katika sekondari ya Janguo kwa kufanikisha upatikanaji wa madawati 87 na hiyo ni kutokana na makubaliano ya wazazi ambao kwa hiyari yao waliamua kuchangia Sh 5,000.
More Stories
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima
Dkt.Biteko aagiza Kituo cha huduma kwa wateja Tanesco kusukwa upya