Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo amesema jamii ina jukumu la kumuunga mkono mwanamke mjamzito kuona tangu anapata mimba hadi kujifungua, basi kuwe na ulinzi kuona anajifungua mtoto akiwa salama.
Na jitihada za kuona mwanamke mjamzito anakuwa salama hadi kujifungua, zimeanzishwa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za wanawake na watoto zinaimarishwa nchi nzima kwa kujenga vituo vya afya, zahanati na hospitali.
Aliyasema hayo Mei 25, 2023 kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambapo alikuwa anawaeleza tukio litakalofanyika Mei 28, mwaka huu kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mazoezi.
Zoezi hilo limepewa jina la Korogwe Mamathon, Mwendo wa Mama ili kuihamasisha jamii iweze kumpa ulinzi wa kutosha mama mjamzito ikiwemo kupata huduma za uhakika kwenye vituo vya afya ili mama huyo aweze kujifungua salama.
“Lengo letu la kuanzisha Korogwe Mamathon ama Mwendo wa Mama, ni kuwahamasisha akina mama wanapopata ujauzito basi waone hilo ni jambo la fahari na wanatakiwa kujivunia sababu wanatuletea viumbe hapa duniani.
“Na kwa kutambua Mwendo wa Mama, na sisi tunawajibu wa kumuenzi mwanamke kwa cheo kikubwa cha kuitwa Mama. Hivyo ni lazima mama huyu apate huduma muhimu zitakazomuwezesha kujifungua salama” alisema Mwegelo.
Mwegelo alisema Rais Dkt. Samia ndiyo amempa msukumo wa kuanzisha zoezi hilo la kuwasaidia wanawake wajawazito, kwani ameboresha huduma za afya kwa kujenga miundombinu ya vituo vya afya, zahanati na hospitali karibu nchi nzima, na hata Wilaya ya Korogwe ni wanufaika wa maboresho hayo kwenye Sekta ya Afya.
Tafsiri ya haya yote, ni ule mwendo alioanza nao Mama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni kutambua mchango wa Mama katika kuwatumikia Watanzania na kila kundi ameligusa kwenye jamii. Hivyo na mimi nikaona nimuunge mkono kwa kuanzisha Korogwe Mamathon, Mwendo wa Mama ili kuweza kuwapa huduma nzuri mama wajawazito” alisema Mwegelo
Mwegelo alisema zoezi la Mei 28, mwaka huu siku ya Jumapili, linatarajiwa kuwahusisha wanawake zaidi ya 1,700, ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wanatarajiwa wanawake 1,000, na Halmashauri ya Mji Korogwe wanawake 700.
“Wanawake wanaotaka kuhudhuria wakajiandikishe kwenye vituo vya afya. Tumeelezwa wanawake 700 watatoka Halmashauri ya Mji Korogwe, na 1,000 kutoka Halmashauri ya Wilaya. Kutakuwa na huduma mbalimbali za vipimo ikiwemo virusi vya UKIMWI, shingo ya kizazi, presha, malaria, wingi wa damu, na vipimo vingine” alisema Mwegelo.
More Stories
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu
Jeshi la Polisi Katavi laanika mafanikio 2024