November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT yaanza utekelezaji agizo la Rais Samia matumizi ya nishati safi

Na Joyce Kasiki , Timesmajiraonline,Kasulu

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeanza utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kwa kuanza mkakati wa kutumia nishati mbadala ili kuokoa mazingira

MKUU wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na uharibiu wa mazingira, Jeshi hilo limeanza mkakati wa kutumia nishati mbadala ili kuokoa mazingira.

Brigedia Jenerali Mabena ameyasema hayo alipotembelea Kikosi cha Jeshi 825 Mtabila kilichopo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, ambapo alizindua jiko la gesi katika kikosi hicho.

Alisema lengo ni kuhakikisha vikosi vyote vya JKT vinaachana na matumizi ya kuni ili kuokoa mazingira.

Brigedia Jenerali Mabena ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kimkakati ya Kilimo Mifugo na Uvuvi JKT, alisema Jeshi hilo linahudumia vijana wengi kwa hiyo hata matumizi yake ni makubwa.

“Kwa mwaka mmoja vikosi vya JKT vinahudumia kwa wastani vijana 100,000 ,vijana hawa ni wengi sana hasa kwa matumizi ya nishati ya kuni, kwa hiyo na sisi ni wadau wa kulinda mazingira kwa hiyo lazima tuanze Ä·utoka kwenye matumizi ya kuni kwa ajili ya kupikia na kuanza kutumia nishati mbadala.”alisema.

Amesema ili kutekeleza hilo, JKT iliunda timu iliyoshirikisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo ilifanya tathimini ya kina ya miundombinu ya majiko katika makambi yote ya jeshi hilo.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena kutokana tathmini hiyo, kwa sasa vikosi vinaendela kutengeneza miundombinu ya majiko kwa ajili ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

” JKT inatekeleza kampeni ya kupanda miti katika maeneo ya vikosi na kutumia nguvukazi tuliyonayo kushiriki katika upandaji miti kwenye maeneo ya halmashauri zinazozunguka kambi za JKT ili kuikijanisha Tanzania.”

Naye Kamanda Kikosi 825 Mtabila Luteni Kanali Patrick Ndwenya amesema mradi wa nishati safi ya kupikia umetekelezwa kwa fedha za ndani.

Aidha amesema kikosi hicho kitautumia mradi huo kama shamba darasa kwa vijana wanaopata mafunzo JKT kwa maana ya kuwafundisha namna ya kutunza mazingira kupitia matumizi ya nishati mbadala.
Aidha alisema katika kulinda mazingira, Kikosi kimepanda miti 13,000 ikiwemo miti 1,000 ya matunda.