Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi za Mafunzo ya Kujitolea, likisisitiza kuwa hakuna gharama yoyote ya kupata nafasi hizo, bali zinatolewa kwa vijana waliokidhi vigezo vilivyowekwa.
Akizungumza Leo Januari 20,2026 na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya JKT Chamwino mkoani Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, alisema wazazi na walezi wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya matapeli wanaotumia nafasi hizo kujinufaisha.
Alisema kuwa baada ya kutangazwa kwa nafasi hizo, JKT hupokea taarifa kuwa baadhi ya wazazi wametoa fedha kwa lengo la kupata nafasi hizo lakini hawajafanikiwa. Alisisitiza kuwa nafasi za Mafunzo ya Kujitolea JKT ni bure.
Aidha, Brigedia Jenerali Mabena alisema nafasi hizo zimepelekwa katika ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini kote, ambapo usaili utafanyika kuanzia Januari 26. Aliongeza kuwa watakaochaguliwa wanatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT kuanzia Februari 27 hadi Machi 4 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, JKT linawataarifu vijana watakaopata nafasi za mafunzo hayo kuwa halitoi ajira wala halihusiki kuwatafutia ajira sehemu yoyote ile Bali linawajengea uwezo wa kujitegemea na uzalendo wa Nchi yao.
Alisema sifa na vifaa vya kwenda navyo makambini vinapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.mil.tz.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama