September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKCI, Saudi Arabia yafanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto 30

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

WATOTO 30 wenye matatizo ya moyo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kwa ushirikiano wa madaktari kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo Saudi Arabia na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza wakati wa kuwaaga madaktari hao Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Tatizo Waane, upasuaji huo umefanywa kupitia kambi maalumu ya siku 10 ya uchunguzi na upasuaji wa moyo na kuokoa Sh milioni 700.

Amesema wagonjwa 50 wamefanyiwa uchunguzi na 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na kwamba tangu Saudi Arabia ianze utaratibu wa kuwaleta madaktari wake nchini imetumia Sh bilioni 4.5.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji mkubwa, Esther Msangalawe, ameishukuru JKCI na madaktari hao kwa huduma hiyo ambayo imerejesha mafumaini ya kuendelea kuishi kwa watoto wao.

“Mwanangu ana miaka mitano na aligundulika kuwa na tundu kwenye moyo na mirija yake ya damu ilikuwa membamba, haikuwa rahisi lakini tunashukuru sana kwa msaada huu,” amesema Msangalawe ambaye ni mkazi wa mkoani Mbeya.

Kwa upande wake Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bin Ahmed Okeish, amesema mpaka sasa zaidi ya watoto 300 wamenufaika kupitia mpango huo.

Aidha amesema kupitia programu hiyo watu 6,898 katika nchi 169 duniani wamenufaika huku ikigharimu Dola za Marekani bilioni 108.