Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma,ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi na upasuaji pamoja na kufulia katika kituo cha afya Kayenze wilayani Ilemela,ambao utagharimu kiasi cha zaidi ya milioni 300(314,747,590.00).
Mara baada ya kumaliza kuweka jiwe hilo la msingi Geraruma ameeleza kuwa mradi huo ni mzuri huku akitaka wataalamu wa Halmashauri washirikishwe katika kamati za maendeleo ya miradi.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary,Dkt.Robert Nenetwa,wakati wa uwekwaji wa jiwe la msingi kupitia Mwenge wa Uhuru ambao kwa mwaka huu una kauli mbiu isemayo”sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo,shiriki kuhesabiwa tuyafikie maendeleo ya taifa”.
Ameeleza kuwa,ujenzi wa jengo ya wodi ya wazazi na upasuaji umefikia asilimia 92 huku ujenzi wa jengo la kufulia umefikia asilimia 92.
Dkt.Nenetwa ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kupunguza vifo vya kina mama na watoto pamoja na kupunguza msongamano katika kituo cha afya Karume,hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure na hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando pamoja na kupunguza umbali wa wananchi kutoka visiwani kufuata huduma za afya.
“Mradi huu hadi kukamilika utagharimu jumla ya milioni 314.74(314,747,590.00, ambapo hadi sasa jumla ya milioni 284.4(284,447,402.00),zimetumika kwa mchanganuo wa fedha za tozo kutoka Serikali Kuu milioni 250,fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri milioni 33.4(33,429,250.00) na nguvu za wananchi milioni 1.0(1,018,152.00),”ameeleza Dkt.Nenetwa.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula, ameeleza kuwa wananchi wa Kayenze wana historia ya muda mrefu ya kufuata huduma ya afya.
Ambapo walikuwa wakitembea umbali mrefu na wengine walikuwa wanatoka kisiwani kwa ajili ya kufuata huduma hiyo ya afya Sangabuye na maeneo mengine.
“Kwa niaba ya wananchi wa Ilemela napenda kutoa shukrani kwa Rais Samia,kwa namna ambavyo anaendelea kuwezesha taifa hili ikiwemo Ilemela na namna serikali inavyojibu hoja za wananchi katika suala la huduma za jamii,”ameeleza Dkt.Angeline.
Wakati huo huo Dkt.Angeline ameeleza kuwa taifa litafanya sensa ya watu na makazi ifikapo Agousti 23 mwaka huu ambapo kwa mara ya kwanza itafanyika sensa ya makazi,hivyo amewaomba wananchi wote kushiriki katika zoezi hilo.
“Taarifa ya majengo yenu,nyumba iwe imekamilika,boma iwe ni msingi lazima utoe kwa sababu lengo la serikali ni kutaka kujua uchumi wa watanzania, uchumi wa mtu mmoja mmoja,lakini ni kwa namna gani mipango ya serikali inaenda kutekeleza kwa kutambua idadi ya watu,” ameeleza Dkt.Angeline.
Awali akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Magu,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, ameeleza kuwa jumla ya miradi 8 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.9(1,938,044,671.80) itatembelewa.
“Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Kata 10 kati ya 19 za Wilaya ya Ilemela kwa umbali wa km 84.1,ambapo miradi miwili itawekwa mawe ya msingi,miradi mitano itazinduliwa na mradi mmoja utakaguliwa,”ameeleza Massala.
Mwenge huo umeweka mawe ya msingi katika miradi ya ujenzi wa jengo la wazazi, upasuaji na kufulia kituo cha afya Kayenze na mradi wa barabara ya TBL kiwango cha lami nyepesi yenye urefu wa mita 900 ambao umegharimu kiasi cha milioni 499.9(499,953,596.20).
Ambapo miradi iliozinduliwa ni ya ufugaji wa samaki kwa vizimba-Igalagala, anwani za makazi na sensa, ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa shule ya sekondari Bujingwa,kituo cha mafuta ASHCO Oil na ujenzi wa mradi wa maji mlima Rada Kiseke huku mradi mmoja ukikaguliwa was shughuli za mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa