December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jitihada za makusudi zahitajika kuokoa uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji

Na Martha Fatael, TimesMajira online

SERIKALI za Tanzania na Kenya zimeombwa kuongeza jitihada za makusudi kuokoa uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji unaofanywa katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Tayari athari za uharibifu wa mazingira zimeonekana katika milima ya Kilimanjaro, Meru, Udzungwa, Uluguru, Same, na Ambuseri ambapo ya maeneo yamepotesa uoto wa asili.

Rai hiyo imetolewa na Viongozi wa kimila wa jamii ya wafugaji wa kimasai wa Tanzania na Kenya wakiwa katika maombi na mafunzo maalumu kuhusu urejeshwaji wa uoto wa asili.

Laigwanani mkuu wa jamii ya wafugaji wa Tanzania, Joseph laizer amesema hayo katika Kijiji Cha Ormelili wilaya ya Siha Kwamba wafugaji wa Tanzania na Kenya wameanzisha kampeni hiyo itakayodumu kwa miaka mitatu.

“Pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, Kuna umuhimu mkubwa kwa serikali za nchi hizi mbili, kuongeza kampeni za kulinda mazingira na vyanzo vya maji,huku zikitolewa adhabu Kali kwa wakaidi” amesema.

Ameziomba serikali za nchi hizo kudhibiti uvamizi unaofanywa na baadhi ya wananchi katika vyanzo vya maji na maeneo ya kimili ambayo husaidia katika hifadhi ya mazingira.

Katika kampeni hiyo iliyoambatana na kupanda miti katika kijiji cha Ormelili wilayani hapa iliyopewa jina la White Mountain ( mlima mweupe) imefadhiliwa na serikali ya Uholanzi.

Naye Laigwanani wa mkoa wa Morogoro, Adam Ole Mwarabu amesema kampeni kubwa inafanyika katika milima ya Uluguru ili kuhifadhi kwa kurejesha miti ya asili na kudhibiti matukio ya Moto.

Kwa upande wake,Mwanzilishi wa kampeni hiyo Frank Heckman kutoka Uholanzi amesema kampeni kama wameifanya nchini Kenya na India ambako imeleta mafanikio makubwa.

Akizindua kampeni hiyo mkuu wa wilaya ya Siha, Christopher Timbuka ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, amesema serikali inaunga mkono kampeni hiyo.

Kadhalika ametaka viongozi hao kuitumia kampeni hiyo kuwahamasisha wazazi wa jamii hiyo kuwapeleka watoto wao shule hoja ambayo iliungwa na kiongozi kutoka Kenya.