Na Israel Mwaisaka,TimesMajira online
UGONJWA wa kifua kikuu nchini bado ni tatizo licha ya kuwapo kwa tiba sahihi,changamoto za matumizi ya dawa kwa muda mrefu ni changamoto kubwa miongoni mwa jamii hasa kwa jamii waishio vijijini.
Kufuatia changamoto hiyo bado kuna Watu wengi ambao wanakimbilia kwa waganga wa jadi kwenda kupata tiba ya kifua kikuu matokeo yake huwa ni mbaya sana,mwishowe hukimbilia hospitali huku ugonjwa huo ukiwa umetengeneza usugu.
Mmoja wa wagonjwa aliyepona ugonjwa huo baada ya kupata tiba stahiki Ivo fidel mkazi wa kijiji cha Namanyere wilayani Nkasi,alidai kuwa yeye baada ya kupata maambukizi ya kifua kikuu alikimbilia kwa waganga wa jadi na hali yake iliendelea kuzorota na ndipo alipokwenda hospitali ambako alikwenda akiwa amechelewa sana na ugonjwa huo kutengeneza usugu.
Alisema kuwa baada ya vipimo kubaini kuwa anamaambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu alianza kupata dawa kutokana na usugu wa ugonjwa huo,alitumia dawa kwa muda mrefu sana kiasi cha kukata tamaa lakini alijitahidi na matokeo mazuri aliyaona baada ya kukamilisha dozi na kwa sasa amepona kabisa.
Amefafanua kuwa wakati wa tiba hiyo kuna mwenzake aliyekuwa wakitibiwa naye aliamua kukimbia na kuacha kuitumia tiba hiyo ya kifua kikuu ,hivyo aliharibu dozi na kwenda kwa mganga wa kienyeji na kuwa baadae alirudi hospitali akiwa na hali mbaya sana na kuwa sasa ameanza upya kuitumia dozi ya ugonjwa huo na sasa afya imeendelea kuimarika na kama asingekatisha dozi hiyo basi hata yeye hadi hivi sasa angekuwa amepona kama yeye.
Janeth Mwita ni mmoja wa waliotibiwa ugonjwa huo na kupona amedai kuwa yeye baada ya kuhisi kuwa huenda ana maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu alikwenda moja kwa moja kwenye vipimo na ikabainika kuwa ana ugonjwa wa kifua kikuu na alianza kupata tiba toka siku hiyo na yeye alitumia muda wa miezi 6 kupata matibabu na kupona kabisa kwa sababu yeye aliwahi kuanza kupata tiba.
Kimsingi ugonjwa wa kifua kikuu unatibika lakini changamoto yake kubwa ipo kwenye matumizi ya dawa kwa muda mrefu ambapo wengi wao huanza kutafuta njia ya mkato ya kutafuta tiba nyingine mbadala ambazo ikiwemo kwa waganga wa kienyeji ambako tiba hiyo haipo na kutengeneza usugu wa tatizo na hata wengine kupoteza maisha.
Tabibu wa ugonjwa huo wa kifua kikuu wa kituo cha Afya Nkomolo wilyani Nkasi mkoa wa Rukwa Deus Msafiri amefafanua kuwa ugonjwa huo umegawanyika katika makundi makubwa mawili ambapo kundi la kwanza ni la mapafu na kifua kikuu cha nje ya Mapafu na kuwa ugonjwa huo unaenezwa kwa njia ya hewa na kuwa mtu yeyote anaweza kuambukizwa bacteria wa ugonjwa huo wa mapafu.
Kutokana na ufafanuzi wake alidai kuwa ugonjwa huo wa kifua kikuu uligunduliwa hapa hapa Nchini mwaka 1802 katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam na Dkt,Robert Coach Mjerumani na kuwa ugonjwa huo ni wa hatari sana na unaenea kwa kasi kubwa.
Na mgonjwa mmoja mwenye maambukizi ya kifua kikuu kwa mwaka anaweza kuambukiza watu 15 hadi 20 na kuwa idadi hiyo ni kubwa na ni lazima ziwepo jihada za makusudi za kukabiliana na ugonjwa huo kinyume cha hapo janga kubwa laweza kutokea.
Takwimu kwa wilaya Nkasi kwa mwaka jana ilikua na wagonjwa 88 na mwaka juzi walikua 83 na kuwa kasi ya maambukizi bado ni kubwa na idadi hii ni ndogo kutokana na idadi ya Watu wanaokwenda kupima afya kwa hiari na kuweza kutambulika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo wa kifua kikuu.
Katika kuonyesha ukubwa wa tatizo hilo la ugonjwa wa kifua kikuu hapa nchini ni kuwa kati ya Nchi 190 ulimwenguni zenye maambukizi ya kifua kikuu Tanzania imo na kwa Nchi 50 za Afrika na Tanzania pia imo hivyo jitihada a makusudi za kuweza kukabiliana na ugonjwa huo zinahitajika.
Dkt.Msafiri anadai kuwa kwa mujibu wa tafiti ni kuwa mtu mmoja mwenye bacteria wa ugonjwa huo na ambaye hajapata matibabu ana uwezo wa kuambukiza watu wengine wapatao 15 hadi 20 kwa mwaka na kuna watu 154,000 hapa Nchini ambao wamekoswa katika kupata huduma.
Amedai kuwa watu hao waliokoswa wapo miongoni mwa jamii na Wanaambukiza hiyo inaonyesha kuwa kwa mantiki hiyo vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu bado vipo na watu wanaishi navyo kinachotakiwa ni jamii kujenga utamaduni wa kwenda kupima ili kama ukibainika uanze kupata matibabu kabla ya kuwa sugu.
‘’’’kwa mkoa Rukwa tuliwekewa lengo la kuwafikia watu 1000 wenye maambukizi ya ugonjwa huo lakini tuliweza kuwafikia watu 947 wenye maambukizi vya vimelea hivyo vya kifua kikuu kwa mgfono huo pekee inaonyesha tatizo bado ni kubwa’’’’
Kwa nini matibabu ya kifua kikuu yanachukua muda mrefu? Inatokana na ugumu wa mdudu mwenyewe lakini tafiti mbalimbali zimeendelea kufanyika na kupunguza unywaji wa dawa nyingi za siku hadi kupelekea kutumia kidonge kimoja chenye dawa Nne ndani yake.
Akitolea maendeleo ya tafiti za dawa tabibu Msafiri anafafanua kuwa miaka nyuma mgonjwa mmoja wa kifua kikuu alikua anakunywa vidonge 12 kwa siku ikaenda hadi vidonge 4 kwa siku na kuwa maendeleo ya utafiti yalikwenda mbali zaidi hadi kufikia kupatikana kwa kidonge kimoja chenye dawa 4 ndani yake.
Tafiti zaidi zinaendelea na kubwa linalofanyika sasa ni kutaka kuona changamoto ya tiba ya muda mrefu inatoweka lakini kwa sasa tiba iliyopo ni sahihi na inatibu kiuhakika.
Tiba ya muda mrefu imewafanya wengi ya Waganga mataperi kuwashawishi wagonjwa waone kuwa wamelogwa ili wawee kwenda kupata tiba kwao kwa lengo la kujipatia kipato huku wakijua kuwa wao hawana uweo wa kuutibu ugonjwa huo.
Jamii inachotakiwa kujua ni kuwa hakuna mahala pengine nje ya hospitali unapoweza kupata matibabu ya kifua kikuu,kwani tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hakuna mganga wa kienyeji aliyewai kuweza kuutibu ugonjwa huo lakini kubwa ni jamii kujenga utamaduni wa kupima afya kila wakati hasa vipimo vya kifua kikuu ili kuweza kujilinda kwa kupata matibabu haraka pale inapobainika una vimelea vya ugonjwa huo.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani