Na Penina Malundo, TimesMajira Online, DSM
LICHA ya juhudi za serikali, kuhakikisha wanawaondoa watu hofu kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 mapema Machi mwaka 2020, bado waathirika wa magonjwa kama Kifua Kikuu (TB) na Virusi vya Ukimwi (VVU) walikuwa na wakati mgumu wa kuhakikisha wanajilinda ili wasipate maambukizi.
Wagonjwa pamoja na wauguzi wa vituo mbalimbali vya kutoa huduma za afya na tiba walijitahidi kuhakikisha huduma za utolewaji wa dawa kwa wagonjwa zinabaki palepale huku hatua mbalimbali zikichukuliwa.
Na hii sio kwa Tanzania pekee, hata katika nchi nyingine ambazo zilikuwa zimezuia mikusanyiko ya watu na kufunga mipaka yake lakini bado walikuwa wanajitahidi kuhakikisha wagonjwa wa kifua kikuu ‘TB’ na VVU wanapatiwa dawa.
Mmoja wa wagonjwa wa TB na VVU, Halima Hassan (sio jina lake halisi), anasema kipindi cha Covid-19 kilikuwa ni kipindi cha kikwazo kwao kwani walilazimika kukaa nyumbani muda mwingi ili kuepuka msongamano wa watu.
Hii ni kutokana na wao kuwa miongoni mwa wale wanaoweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa haraka. Anasema uwepo wa Covid-19 ulibadili hata mfumo wa upataji dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi ‘ARVS’ na TB.
Anasema moja ya njia zilizotumika ilikuwa ni kuanzisha vituo vya dharura, ambapo walikuwa wanakwenda kuchukua dawa kwa watendaji kata au vituo vilivyo karibu na maeneo wanayoishi.
Hassan anasema licha ya uchukuaji wa dawa kwa watendaji wa kata kuonekana njia rahisi, bado iliibua unyanyasaji kwa jamii inayowazunguka baada ya wahusika hususani wale ambao walikuwa hawatambuliki kujulikana kuwa wanamaambukizi ya VVU.
Anasema hali hiyo haikuwarudisha nyuma wagonjwa kwenda kuchukua dawa na kuhakikisha wanajikinga na Covid-19.
“Njia nyingine tuliyokuwa tunapatiwa ilikuwa ni kutoa dawa za muda mrefu kwa miezi mitatu hadi sita kulingana na sehemu anayoishi mtu na hali yake ilivyo,” anasema na kuongeza
“ Lengo la kupewa dawa za muda mrefu lilikuwa ni kuhakikisha wagonjwa hao wanakuwa salama na kuepuka maambukizi,”alisema
Pudensia Mbwiliza ni mmoja wa watu wenye maambukizi ya Ukimwi. Anasema taarifa ya kwanza ilipoingia kuhusu ugonjwa wa Korona aliingiwa na hofu kubwa.
Mbwiliza anasema taarifa ya ugonjwa huo iliwapa mshtuko, ila baada ya kujua hali zao walikuwa wanapunguza hali ya kukaa kimsongamano.
Anasema baada ya kupata taarifa sahihi kuhusu Covid-19, kila kitu kilikuwa vizuri na kuanza kuondoa hofu na akapata kuendelea na harakati zake kama kawaida.
Aidha, anasema katika kituo cha afya ambacho anapatiwa dawa mara nyingi watoa huduma wa kituo hicho walikuwa wanawahimiza wagonjwa kutokaa karibu karibu na kuhakikisha wananawa mikono yao mara kwa mara.
Awali, walikuwa wanamazoea ya kukaa na kuongelea masuala ya Ukimwi, badala yake walipunguza hali ya msongamano. Anasema ilikuwa ukitoka kwa daktari unakuta dawa tayari zimewekwa, hivyo hali ya mzunguko wa muda mrefu kama kipindi cha kabla ya Covid-19 ilikuwa haipo.
“Tulikuwa tunajitahidi kuelimishana wenyewe kwa wenyewe juu ya kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu ikiwemo unawaji wa mikono mara kwa mara, pamoja na kukaa kwa umbali,” anasema Mbwiliza.
Anasema aliishi katika mazingira magumu kwa sababu hakujua hatima yake ya maisha itaishia wapi kwa sababu kila siku walikuwa wanapokea taarifa mpya juu ya ongezeko la wagonjwa wa Covid-19 na vifo.
Naye Prisca Alonas(sio jina lake halisi) anasema kipindi cha Covid-19 changamoto kubwa aliyokumbana nayo ni pamoja na kuvaa barakoa kwani hakuwa na mazoea hivyo ilimpa shida.
Anasema watu walikuwa wanaogopa hali ambayo ilisababisha kuacha kushauriana juu ya masuala ya VVU kwa sababu kila mtu alikuwa na hofu.
“Maisha yalikuwa magumu sana kipindi kile ukizingatia mimi ni mjasiliamari mdogo nauza maandazi, chapati na vitumbua sasa fedha za kununulia limao na tangawizi ilikuwa ni ngumu sana kwangu hivyo nilikuwa ninahofu sana na maisha yangu kipindi chote,” anasema.
Daniel Ilulu(sio jinalake halisi) ni miongoni mwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi anasema kuwa alianza kununua malimao ili watumie na familia yake. Hali ya kununua bidhaa hizo zilikuwa zikimgharimu sana kwani hakuwa anatumia peke yake bali familia nzima huku limao moja lilikuwa likiuzwa kwa kiasi cha sh.1000 hivyo ilikuwa ni ngumu kwao kujikimu katika maisha ya kawaida.
“Ilikuwa ni ngumu sana katika kipato chetu kujikimu kimaisha kwani nilikuwa natoa fedha nyingi ili watu wote wa nyumbani waweze kupata limao, tangawizi na haya majani ya kujifukiza ukizingatia na mke wangu nae anaishi na virusi vya Ukimwi,” anasema na kuongeza,
“Kwa upande wa hospitali tuliambiwa wenye virusi chini ya 50 wangekuwa wanatuletea dawa karibu na nyumba zetu, na tulikuwa tukipigiwa simu na kuelekezwa aina ya gari lililopo na gari hili lilikuwa likitolewa nembo, hivyo tulikuwa tukielekezwa kwa simu hadi tutafika,” anasema.
Ilulu anasema walikuwa wanapewa dawa za miezi sita sita wanapoenda kwenye gari kuchukua kipindi chote cha Covid-19.
“Mara ya kwanza waliponipigia nikachukue dawa karibu na nyumbani kwangu nilikuwa na hofu kubwa ya watu kuja kunigundua kama mimi ni muathirika ila nilikuwa nauliza mazingira yapoje lakini walikuwa wanatupatia dawa walitutia moyo na kutuondoa hofu kuwa hakuna watu ambao wangeweza kutugundua,” anasema Ihuri.
Hata hivyo, Ilulu anasema kwa sasa wamerudi kituoni wanapopatiwa tiba na kuendelea na huduma mbalimbali, ikiwemo kuchukuliwa vipimo vya kuangalia idadi ya virusi walivyokuwa navyo.
MADAKTARI, WAHUDUMU WA AFYA WANANE
Kwa upande wake, Daktari Bingwa Magonjwa ya Ndani na Mkuu wa kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Amina Mgunya, anasema walihakikisha wagonjwa wanakuwa na dawa za kutosha.
Awali ilikuwa watu wanapewa dawa za mwezi mmoja mpaka mitatu, lakini kipindi cha mlipuko wa Corona waliruhusu wagonjwa kupewa dawa mpaka za miezi sita.
“Hatua hiyo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mkusanyiko wa wagonjwa waliokuja kufuata dawa na kwa jinsi ilivyotokea mwezi ule wa tatu na wa nne, kwa kuwa pia tulikuwepo katika kitengo cha kupambana na Covid-19 hatukupata sana wagonjwa wenye Korona na VVU,” anasema.
Hata hivyo, kliniki zilikua zikianza mapema zaidi ili kuepuka mikusanyiko ya wagonjwa wengi na katika ukaaji wakati wakisubiri huduma wagonjwa walilazimika kukaa umbali wa mita moja.
“Tuliruhusu treatment supporters (wasaidizi wa matibabu) kuja kuwachukulia wagonjwa dawa hasa wale ambao wana umri mkubwa au wana magonjwa mengine,” anasema.
Aidha Dkt Zainabu Mwinyimkuu, Mkuu wa Kitengo cha Care Treatment Center (CTC) kilichopo Chanika, Dar es Salaam kinachohudumia wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na wenye Virusi vya Ukimwi (VVU), anasimulia namna ambavyo waliweza kufanya kazi kwa kipindi hiko.
Anasema moja ya njia ambayo waliigundua ili iwasaidie wagonjwa hususani wa TB ni kuwafuata wagonjwa wao maeneo ya karibu na majumbani na kuwapigia simu kuja kuwapa dawa.
Dkt Mwinyimkuu anasema mbinu hiyo ilionekana kuwavutia wagonjwa ambao walikuwa na hofu ya kufuata dawa katika kituo chao cha tiba cha Chanika, kutokana na kuhofia kuambukizwa Corona pindi wanapopanda mabasi.
“Tulibuni njia hii baada ya kuona wagonjwa wakilalamika namna ya kufika kliniki kutokana na usafiri wanaotumia kwa daladala kuhofia kupata maambukizi,” anasema.
Dkt Mwinyimkuu anasema kwa upande wa wagonjwa ambao wana TB na VVU kwa pamoja, waliweza kufika katika kituo hicho asubuhi mapema na kupatiwa matibabu kama kawaida, huku wakihakikisha wanawapatia maelezo yote ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Korona.
“Tulihakikisha wanapoingia kituoni wananawa mikono yao na maji tiririka pamoja na sabuni huku katika sehemu za kukaa walikuwa wakizingatia umbali kati ya mtu mmoja na mwingine,” anasema.
Vilevile anaeleza kuwa vituo hivyo walivyobuni viliweza kuwasaidia kidogo, huku wachache wakiamua kuchukua dawa katika vituo vyao vya jirani.
Anasema katika kituo chao walikuwa wanapokea wagonjwa hata wanaotoka sehemu nyingine kwa ajili ya kupata matibabu hapo na waliweza kuwapatia matibabu sawa na wale wanaohudumiwa katika kituo chao.
“Kipindi cha Corona tulikuwa tukijitahidi kuelimisha wagonjwa wa TB kuhakikisha wanafuata elimu inayotolewa na wataalamu wa afya na wala hatukufunga vituo vyetu vya afya. Wagonjwa walikuwa wanakuja kama kawaida,” anasema na kuongeza,
Kwa upande wa watoto wadogo wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, Dkt Mwinyimkuu anasema katika kipindi hicho cha Corona, wao walikuwa wanaenda katika kliniki zao kama kawaida, kwa kuzingatia hatua zote za kujikinga na ugonjwa wa Corona na kuzifuata.
Anasema kikubwa kwa watoto wenye maambukizi hayo ya Ukimwi na TB mara nyingi walikuwa hawawapatii dawa nje ya kituo chao cha kutolea dawa.
Watoto wadogo dawa zao hupatiwa kulingana na uzito wao, hivyo ni lazima uwiano wa uzito uendane na utoaji wa dawa ya kuzubaisha virusi kwa watoto hao.
Dkt. Mwinyimkuu anasema watoto wanakuwa wapo katika hatua ya kawaida mara nyingi hukutana nao katika kituo chao ndani ya kipindi cha miezi sita, huku kwa watoto ambao wapo katika hali dhaifu sana hawa walikuwa wanakutana nao kwa kila baada ya mwezi mmoja.
Aidha, anasema kipindi chote hicho walivyokuwa wanatoa dawa hususani katika zoezi la kuwafuata wagonjwa maeneo ya karibu na majumbani kwao walikuwa wanazingatia hali ya faragha ambapo walikuwa wanatoa dawa bila mtu yoyote kujua.
“Tunapokuwa tunaenda kupeleka dawa tunahakikisha sehemu tunayokaa ni sehemu ya utulivu ambayo tunahakikisha hakuna watu wanapitapita na kujua kama wanapewa dawa,” anasema Mwinyimkuu.
TAKWIMU ZINASEMAJE JUU YA HALI YA VVU
Taarifa ya UNAIDS ya mwaka 2018 inaonesha kuwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vimepungua kwa asilimia 49, kutoka 48,000 hadi 24,000, huku idadi ya maambukizi mapya pia ikipungua kutoka 83,000 hadi 72,000 katika kipindi hicho hicho.
Hata hivyo wanawake wameathiriwa zaidi na VVU nchini Tanzania huku kati ya watu wazima, 880,000 (asilimia 58.67) walikuwa wanawake. Maambukizi mapya ya VVU kati ya wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24 walikuwa zaidi ya mara mbili ya wale wa kiume.
Makala hii imeungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti Majanga.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani