October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jiji la Mbeya, mwekezaji wajadili namna ya kuzalishaji mbolea Dampo la Nsalaga

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MENEJIMENTI ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya imekutana na wawekezaji kutoka Kampuni binafsi ya BA Prerna CleanEarth kujadili uwezekano wa kuwekeza katika dampo la Nsalaga na kuzalisha mbolea inayotokana na taka zinazooza.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo kutoka Gujarat India, Parish Kalathia, amesema endapo Jiji litaridhia, kampuni hiyo itachakata taka hizo kwa kutenganisha taka ngumu na zile zinazooza na kisha kuzalisha mbolea zinatotumika shambani.

Amesema mbolea inayotokana na taka zinazochakatwa haitakuwa na madhara yoyote kwenye ardhi na mimea itakayozalishwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya,John Nchimbi amesema Jiji limepokea ombi hilo la ushirikiano na kueleza kuwa suala hilo litafikishwa ngazi za juu endapo itaridhiwa taratibu nyingine zitafuata ikiwa ni pamoja na kusaini mkataba wa ushirikiano.

Nchimbi amesema uwekezaji kama huo umefanyika Kilimanjaro na Dar es Salaam na kuleta mafanikio.

“Uwekezaji huu mbali ya kuwa chanzo cha mapato endapo utaridhiwa pia utawanufaisha wakulima kwa kupata mbolea bora na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao mbalimbali,” amefafanua Nchimbi.