Na Dennis Gondwe,Timesmajiraonline,Dodoma.
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inajivunia kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wataalam na Baraza la Madiwani katika kusimamia na kudhibiti matumizi sahihi ya fedha.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu na Fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA. David Rubibira alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa miaka mitatu ofisini kwake.
CPA. Rubibira amesema “kwa bahati nzuri kwa kipindi cha uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ikipata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo. Hati inaangalia maeneo yafuatayo.
Ukaguzi wa hesabu zilizowasilishwa na ukaguzi wa vitabu vilivyofanya malipo, nyaraka, viambata vyote na mchakato wa ukusanyaji mapato kama ulizingatia sheria, kanuni na taratibu. Hivyo, hati safi inatokana na muunganyiko wa hesabu kwamba umefuata viwango vya kimataifa na kuonesha ukweli” alisema CPA. Rubibira.
Amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano baina ya wataalam na Baraza la Madiwani.
“Wataalam wanawajibu wa kufuata sheria, kakuni na taratibu za fedha wanapotekeleza majukumu yao na waheshimiwa madiwani wanawajibu wa kuisimamia halmashauri ili iweze kutekeleza majukumu yake.
“Hivyo, ushirikiano huu ndio unapelekea halmashauri kupata hati safi”amesema CPA. Rubibira.
Mafanikio mengine alitayaja kuwa ni katika eneo la ukusanyaji mapato ya ndani.
“Mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri ilikisia kukusanya jumla ya shilingi 43,616,465,99, lakini iliweza kukusanya makusanyo halisi shilingi 44,279,552,980 sawa na asilimai 102. Mwaka wa fedha 2022/2023 halmashauri ilikamisia kukusanya shilingi 55,127,359,997 lakini iliweza kukusanya makusanyo halisi shilingi 44,639,819,472.12 sawa na asilimia 81. Mwaka 2023/2024 halmashauri ilikamsimia kukusanya shilingi 58,640,360,000 mpaka kufikia mwezi Machi, tumeshakusanya shilingi 32,760,459,121 sawa na asilimia 54.7.
Kwa mikakati ambayo halmashauri imejiwekea kufikia tarehe 30 Juni, tunatarajia kuwa tumefikisha asilimia 100 ya makusanyo halisi”amesema CPA. Rubibira.
Akiongelea mapokezi ya fedha za miradi ya maendeleo,amesema kuwa shilingi 29,654,533,199 zilipokelewa kutoka serikali kuu na wadau wa maendeleo.
“Fedha hizo zilitekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya, vyumba vya madarasa, ujenzi wa shule, vituo vya afya, zahanati, nyumba za watumishi na matundu ya vyoo.
Fedha hizo zilisaidia sana katika kuchochea maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akiongelea ukusanyaji wa mapato ya ndani alisema kuwa yanakusanywa vizuri. “Ndugu waandishi wa habari, ukusanyaji wa mapato ya ndani unakwenda vizuri.
Asilimia 40 inatumika kuendesha halmashauri na asilimia 60 inatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo tumeweza kutenga jumla ya asilimia 60 ya mapato ya ndani tuliyokusanya kwenda kwenye miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na asilimia 10 kwenye mfuko wa maendeleo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Fedha za miradi ya maendeleo zimepekwa kwenye uchangiaji wa ujenzi wa barabara, kujenga vituo vya afya, madarasa na zahanati, ofisi za kata na mitaa.
Hivyo, unaweza kuona kwa kiasi gani mapato ya ndani yamechangia kuleta maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu” alisisitiza CPA. Rubibira.
Mkuu huyo wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu aliwashukuru wananchi kwa kulipa kodi na tozo za halmashauri kwa hiari na kwa wakati.
Aliahidi kuwa halmashauri itaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya Habari, matangazo na mikutano mbalimbali ili wananchi wapate elimu ya aina ya kodi na tozo za halmashauri wanazotakiwa kulipa ili waweze kulipa kwa hiari.
“Hivyo, niwasihi wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari, shughuli zote za maendeleo mnazoziona katika jamii ni matokeo ya kodi zenu.
Wananchi mkiona wanafunzi wanaenda kwenye shule nzuri, madarasa mazuri, wanakalia madawati, wakienda hospitali huduma nzuri, dawa zipo mashine za vipimo zipo, ndiyo matunda ya ulipaji kodi” alisema CPA. Rubibira kwa tabasamu.
Aidha, aliwataka kudai risiti ya mashine ya kielekroniki (EFD) wanaponunua bidhaa.
“Ndugu waandishi wa habari, nisisitize kwa wananchi wanaponunua bidhaa kuhakikisha wanapewa risiti za kielektroniki (EFD) na kama wanalipa tozo za halmashauri wahakikishe wanapata risiti ya POS” alisisitiza CPA. Rubibira.
Kitengo cha Uhasibu na Fedha kina jukumu la kukusanya maduhuli ya serikali na kusimamia matumizi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu