

Na Joyce Kasiki ,Timesmajira Online, Mbeya
JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mbeya limeendelea kutoa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa wananchi, likitumia maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Uhindini, Mbeya kama jukwaa muhimu la kufikia jamii.
Akizungumza na waandoshi wa habari katika banda la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Afisa Habari Msaidizi wa Jeshi hilo, Sajenti Ester Kinyaga, amesema ushiriki wa Jeshi hilo kwenye maadhimisho hayo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo kuhakikisha wananchi wanapata uelewa sahihi wa namna ya kujikinga na majanga ya moto pamoja na hatua za kuchukua pindi ajali hizo zinapotokea.
“Kama Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, tupo hapa kuwapatia wananchi elimu ya kinga dhidi ya majanga ya moto. Hii ni nafasi nzuri kwa sababu hapa kuna mkusanyiko mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali,” amesema Sajenti Kinyaga.
Katika banda lao la maonyesho, Jeshi hilo limeweka vifaa mbalimbali vinavyotumika kwenye shughuli za uokoaji, ambapo wananchi wanaopata fursa ya kutembelea banda hilo wanaweza kujionea na kufahamu matumizi ya vifaa hivyo pamoja na majukumu ya Jeshi hilo kwa ujumla.
Sajenti Kinyaga amewahimiza wananchi kufika kwa wingi kwenye banda hilo ili wapate elimu muhimu, ikiwemo kutambua ishara za moto, namna ya kuzuia majanga hayo na hatua za haraka za kuchukua iwapo moto utatokea.
Aidha, amesema,kwa watakaofika kwenye banda hilo watafundishwa kuhusu njia sahihi za kutoa taarifa za dharura kupitia namba ya simu ya bure ya 114, ambayo inatumika kuwasiliana moja kwa moja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Akizungumzia baadhi ya sababu zinazochangia matukio ya moto, Sajenti Kinyaga ametaja uzembe kama chanzo kikuu, akieleza mfano wa watu wanaoacha pasi ya umeme ikiwa imewashwa hata baada ya umeme kukatika, na moto kuzuka pindi umeme unaporudi. Aidha, alionya dhidi ya vitendo vya hujuma vinavyotokana na chuki baina ya watu, hali inayosababisha baadhi ya watu kuchoma mali za wengine kwa makusudi, ikiwa ni pamoja na nyumba au magari.
Jeshi hilo limeendelea kusisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa na uelewa wa masuala ya usalama na tahadhari dhidi ya moto, ili kuokoa maisha na mali kabla ya madhara kutokea.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama