December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jenista Mhagama, waziri mwenye uzoefu utakaoleta mageuzi Wizara ya Afya nchini

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

WIKI iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo ameweka wazi kwamba ni ya kawaida na yanalenga kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Mabadiliko hayo yamekuwa gumzo kubwa huku baadhi ya Watanzania wakihoji sababu za mabadiliko hayo ya mara kwa mara. Lakini ukiangalia kwa jicho la karibu unaona wazi kwamba Rais Samia analenga kuongeza ufanisi kwa kuwa na mawaziri mahiri kwenye wizara nyeti ambao wataweza kutumikia Watanzania ipasavyo.

Miongoni mwa mawaziri ambao wamebadilishwa Wizara Jenesta Mhagama, ambaye Alhamisi wiki iliyopita ameapishwa kuwa Waziri wa Afya akichukua nafasi ya Ummy Mwalimu, ambaye ameachwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Kabla ya uteuzi huo wa wiki iliyopita Waziri Mhagama amekuwa waziri katika wizara mbalimbali ambazo aliziongoza kwa mafanikio makubwa. Kabla ya mabadiliko ya wiki iliyopita, Waziri Mhagama alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Kwa zama za sasa, Mhagama ndiye mwanamama mzoefu kisiasa kuliko wote kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Samia.

Kwenye baraza hilo hakuna mwanamama ambaye amekuwa mbunge kwa zmiaka takriban 19 kama yeye na pia hakuna mwanamama ambaye amekuwa na uzoefu wa uongozi wa juu ndani ya Bunge kwa miaka tisa kama alivyo yeye, hivyo hiyo ni dalili kwamba Rais Samia hajakosema kumteua kuwa Waziri wa Afya.

Pili, Mhagamaa anao uwezo mkubwa wa ujenzi wa hoja na kushawishi. Kwenye Bunge ni mmoja wa wabunge wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja na ushawishi kutoka upande wa CCM na hasa kwenye eneo la wanawake.

Hayo yamemfanya aendelee kuwa na nguvu kubwa kwa wananchi anaowaongoza jimboni hadi ndani ya Serikali.

Huyu kwa sasa hajifunzi siasa, hajifunzi majukumu ya waziri, ana uwezo na fursa na kila sifa ya kufanya vizuri kwenye wizara hiyo na watu wayaone matokeo yake. Tatu, Jenista ni mwanamama anayeyajua mazingira ya watu wa chini na hali hiyo itamsaidia sana kipindi hiki anapoenda kumsaidia Rais Samia kwenye Wizara ya Afya.

Amekuwa mwalimu kwa miaka kadhaa na amefanya kazi katika halmashauri kwa miaka kadhaa. Huyu ni mtu anayejua nini Watanzania wanataka. Akisaidiwa na watendaji wengine Wizarani anaweza kabisa kujenga msingi mzuri ya Watanzania kupata huduma bora za afya.

Rais wa awamu nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi akichukua nafasi ya Philipo Mulugo. Januari 2015 alihamishwa wizara na kuteuliwa kuwa waziri kamili kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge).

Jenista amedumu kwenye wizara hiyo hadi kumalizika kwa uongozi wa JK. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Jenista alichukua fomu ndani ya chama chake na dalili zilianza kujionyesha mwanzo kwamba hakuwa na washindani thabiti.

Siku ya upigaji kura za maoni, washindani wake ambao ni Lazaro Bunungu, mfanyakazi wa Tanroads mkoani Tanga na Clement Makaburi Mwinuka, mwananchi wa kawaida aishiye Peramiho, hawakutokea.

Ilidaiwa kwamba wa kwanza alianguka siku moja kabla ya uchaguzi huo na wa pili fomu yake ilisainiwa na mtu mwingine. Jenista akapita bila kupingwa.

Kwenye Uchaguzi Mkuu, Jenista alishinda kwa kura 32,057 dhidi ya mgombea Chadema, Erasmo Mwingira, jambo lililompa nafasi ya kuwa mbunge kwa kipindi cha nne.

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 mwaka jana, Rais John Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu. Lakini pia baada ya Rais Samia kuapishwa kushika wadhifa huo Machi 2021, ameendelea kuamini utendaji kazi wake na kila wizara aliyomteua kuongoza, ameweza kufanya vizuri, hivyo Rais Samia hajakosea kumpa Wizara ya Afya.

Mhagama ambaye alizaliwa Juni 23, 1967 wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 unakaribia, akiwa na miaka 33, Jenista ambaye ni mwanachama wa CCM wa muda mrefu, alichukua fomu za kuomba ubunge wa viti maalum upande wa ubunge.

Alipambana ndani ya chama chake na kupitishwa na vikao vya juu vya CCM kuwa mbunge kutoka Mkoa wa Ruvuma.

Uzoefu wa miaka mitano ya ubunge ulimpa kila sababu ya kuingia kwenye ubunge wa jimbo kuchuana na wanaume. Mwaka 2005, alisimamishwa na CCM kuwani ubunge katika jimbo la Peramiho.

Katika uchaguzi huo aliwashinda wagombea kutoka CHADEMA, CUF na TLP kwa zaidi ya asilimia tisini ya kura zilizopigwa. Alipata kura 46,480 sawa na asilimia 93.2 na kuwaacha wagombea wa vyama hivyo vitatu wakigawana asilimia 6.8 ya kura zote.

CCM ilimpa Mhagama heshima ya kuwa mmoja wa wenyeviti wa Bunge, nafasi ambayo ni nadra kwa wanawake kutokana na mfumo wa mitandao na nguvu kubwa za wanaume kisiasa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Jenista alishinda kwa mara ya pili kura za maoni ndani ya CCM na kupitishwa kuwa mgombea. Alishindana na mgombea pekee kutoka CUF, Emmanuel Chilokota na safari hii ushindi wake ulipungua baada ya kupata kura 28,782, sawa na asilimia 89.43 akimuacha mgombea wa CUF ambaye alikuwa na kura 2,642, sawa na asilimia 8.21.

Baada ya ushindi wa ubunge wa mwaka 2010, CCM ikampa heshima tena Jenista, akapewa uenyekiti wa Bunge na kuwa mmoja kati ya wafanya maamuzi wakubwa na waendesha vikao maalum vya chombo hicho cha kutunga sheria. Januari 20, 2014

Ndani ya CCM, ameshikilia nyadhifa kadhaa kwa kipindi kirefu. Kwanza alikuwa katibu wa tawi tangu mwaka 1987 hadi 1990, pili amekuwa mjumbe wa Baraza la Wilaya la CCM tangu mwaka 1995 na amewahi kuwa katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) ngazi ya kata kati ya mwaka 1995 hadi 2000.

Matarajio ya Watanzania kwa Waziri Mhagama ni kwamba ataanzia pale alipoishia Ummya Mwalimu na hatimaye ataipeleka mbele wizara hiyo kuondoa vikwazo vilivyomsababisha Watanzania wasipate huduma bora za afya.

Atakuwa anajua kuwa sekta aliyokabidhiwa hivi sasa ina kelele za moja kwa moja kwa sababu imeunganishwa na afya za Watanzania. Kwa msingi huo, hatalala usingizi kwa muda uliobaki kabla ya uchaguzi mkuu 2025.

Watanzania wanatarajia waziri huyu aendeleze mpango na mkakati wa Serikali utakaoisaidia kila Mtanzania kuwa na kadi ya Bima ya Afya . Anatarajiwa achukue hatua atakazoona kweli zinaweza kuhakikisha kila Mtanzania aone umuhimu wa kuwa na kadi ya Bima ya Afya, kwani hilo, ndilo tamanio la Rais Samia.