Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Ni zaidi ya wiki moja sasa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii zilisambaa picha zikionesha jengo la kituo cha polisi Wilaya Butiama mkoani Mara linalodaiwa kujengwa kwa thamani ya milioni 802 ambalo lilizua sinto fahamu na kuibua mijadala mbalimbali kwa wananchi katika mitandao hiyo wakihoji kuwa kiasi kilichotumika akiendani na muonekano wa jengo hilo.
Hali hiyo imeilazimu Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imeunda Kamati inayohusisha
timu za Wahandisi wa ujenzi, wataalam wa ununuzi, Wakadiriaji majengo na Mkaguzi wa Ndani ili kufanya uchunguzi kuanzia ngazi ya ukadiriaji wa gharama za ujenzi hadi hatua ujenzi ulipofikia.
Akifafanua kuhusu suala hilo mbele ya waandishi wa habari mkoani Mwanza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sagini ameeleza kuwa kutokana na gharama kuonekana juu kuliko matarajio ya wananchi wizara hiyo imeamua kuunda kamati kuchunguza ili ipate uhalisia.
Ameeleza kuwa wataalamu wanaojenga kituo hicho ni Jeshi la Polisi hivyo timu iliyoundwa kuuchunguza ni huru na haifungamani na upande wa jeshi hilo wala wizara hiyo.
“Kamati imeundwa tangu Novemba 25,mwaka huu wajumbe watakutana na Katibu Mkuu wa Wizara na kupewa hadidu za rejea ili waanze uchunguzi ifuatilie kwa kina na kujiridhisha kilichofanyika ni halali na kama pana upungufu au uongezaji wa gharama husio halali wahusika wachukuliwe hatua stahiki,”ameeleza Sagini.
Hata hivyo amefafanua kuwa milioni 802 ambayo ni fedha ya makadirio ya ujenzi, tayari Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeshatoa kiasi cha milioni 500 kati ya hizo milioni 366 zimeshatumika kwenye ujenzi wa kituo hicho.
Pia ameeleza kuwa kamati hiyo iende mbele zaidi kwenye utekelezaji wa mradi kama zile fedha zilizotolewa na vifaa vilivyoingia kwenye ujenzi vinakidhi viwango na inaendana na thamani ya fedha iliyotolewa na hakuna upungufu wa maadili na uadilifu uliotekelezwa na wataalamu na wasimamizi wa ujenzi.
Hivyo amewaomba wananchi kuwa na subira kama wizara hawawezi kikubali Rais Samia Suluhu Hassan aangaike kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miradi ya kuwasaidia polisi kuwa na mazingira bora ya kufanya kazi halafu watokee watu au mtu aliyelenga kujinufaisha.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi