January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jela miaka mitano kwa kuiba mtoto

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza

Mahakama ya Wilaya ya Magu,mkoani Mwanza, Septemba 2,2024 imemhukumu kifungo cha miaka mitano jela, Mkazi wa Kisiwa cha Kamasi, Wilaya ya Ukerewa mkoani humo, George Gresheni Mlano baada ya kumkuta na hatia ya kuiba mtoto, mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu (jina linahifadhiwa).

George ametiwa hatiani katika kesi hiyo ya jinai namba 25001 ya mwaka 2024,baada ya kufikishwa katika Mahakama hiyo na kusomewa shtaka la wizi wa mtoto na Wakili wa Serikali, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Nuru Julius Nnko mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Erick Kimaro.Ambapo mshitakiwa baada ya kusomewa shitaka hilo alikiri kutenda kosa hilo.

Wakili Nuru amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 169 (1)(a)na (b)Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya sheria marejeo ya mwaka 2022.Na kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 10,2024,kitongoji cha Wita, Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Hata hivyo baada ya kutenda kosa hilo, Jeshi la Polisi Agosti 16,2024 lilifanikiwa kumkamata mshitakiwa huyo, Kisiwa cha Gana Wilaya ya Ukerewe akiwa na mtoto huyo, ambapo taarifa ya kukamatwa kwake ilitolewa na kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafugwa Agosti 23,2024.