November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wawili jela miaka 21 kwa uvunjaji na wizi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imewahukumu vijana wawili, Hamisi Kwabi (22), na Mohamed Kassim (22) kifungo cha miaka 21 jela baada ya kukiri makosa matatu ya kuvunja na kuiba kwa miezi tofauti.

Waliohukumiwa adhabu hiyo wakazi wa Mtaa wa Stoo kata ya Igunga kutumikia adhabu ya

Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba alidai mahakama mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, Lydia Ilunda kuwa katika shtaka la kwanza washtakiwa wote walitenda kosa hilo Februari 6, 2021 usiku.

Aliongeza kuwa washtakiwa walivunja nyumba ya Onanis Jackson mkazi wa Mtaa wa Kamando kwa nia ya kuiba kinyume na kifungu 294(1)(a)(2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2019.

Alidai baada ya kufanikiwa kuingia katika nyumba hiyo waliiba TV aina ya Boss yenye thamani ya sh 1,100,000, kompyuta mpakato aina ya HP yenye thamani ya 900,000, feni yenye thamani ya sh. 45,000 vyote vikiwa na thamani ya sh 2,045,000.

Alidai kosa hilo ni kinyume na kifungu 265 na 258 (1) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2019.

Majid alidai shitaka la pili ni kuvunja nyumba usiku kwa niaba ya kuiba kinyume na kifungu 294(1)(a)(2) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2019, ambapo Februari 11/2021 muda wa usiku katika Mtaa wa Masanga Mjini Igunga washitakiwa wote wawili walivamia na kuingia kwenye nyumba ya Hanifa Thabit.

Majid alibainisha kuwa baada ya kuingia walifanikiwa kuiba television aina ya Boss yenye thamani ya sh. 900,000, ambapo walitenda kosa hilo kinyume na kifungu 265 na 258 (1) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2019 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Mwendesha mashitaka huyo alidai shtaka la tatu kwa washitakiwa hao wawili ni kuvunja nyumba usiku kwa nia ya kuiba kinyume na kifungu 294(1)(a)(2) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio 2019.

Majid aliendelea kuiambia mahakama kuwa machi 27/2021 majira ya usiku katika mtaa wa Kamando mjini Igunga washtakiwa baada ya kufanikiwa kuvunja nyumba ya Khalfani Mohamed waliiba television moja aina ya Samsung yenye thamani ya sh. 800,000 na walitenda kosa hilo kinyume na 265 na 258(1) kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2019.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo matatu mbele ya Hakimu Lydia Ilunda washtakiwa hao walikiri makosa.

Aidha kabla ya kutoa hukumu, Mwendesha Mashitaka aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa kwa kuwa wamekuwa tishio kwa uvunjaji wa nyumba na kuiba katika mji wa Igunga kwa muda mrefu.

Akitoa hukumu kwa washtakiwa Hakimu wa Wilaya Lydia Ilunda amesema kutokana na washtakiwa kukiri makosa yao matatu na upande wa mashtaka kuthibitisha vitendo vilivyofanywa na watuhumiwa hao, mahakama imeona pasipo ubishi washtakiwa wana hatia hivyo kwa makosa hayo matatu kila moja miaka 7, hivyo kwa yote miaka 21 ili iwe fundisho kwa wengine.