November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jasco kukamilisha ukarabati wa barabara jijini Mwanza

Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Mwanza.

KAMPUNI ya kizalendo ya Jassie company Ltd(Jasco) imesema hivi karibuni itahakikisha inakamilisha ukarabati wa barabara zilizopo Kata ya Mahina na Mirongo jijini Mwanza.

Hayo yamebainishwa Januari 18,2024 na Mhandisi wa kampuni hiyo Mhandisi Justine Kaundama wakati akizungumza na waandishi wa habari waliomkuta kazini akiendelea na ukarabati wa madaraja ili kuwawezesha wananchi kufanya kazi zao.

Ambapo amsema wamefanya kazi mchana na usiku ili kurudisha miundombinu vizuri licha yà mvua kubwa kuendelea kunyesha kila siku lakini Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA)kwa kutumia kampuni za kizalendo hapa nchini imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha maeneo yanapitika muda wote.

Amesema madaraja na makaravati ambayo yalikuwa yamesombwa na maji kwenye maeneo tofauti yameweza kurudishwa kwenye hali nzuri kufuatia jitihada zinazofanywa katika maeneo tofauti jijini Mwanza.

Akishuhudia kazi hiyo mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Mwananchi,Juma Ali amesema kuwa daraja la Mwananchi lilikuwa limekatwa na maji lakini wameona namna serikali ilivyo tatua tatizo hilo kwa kutoa fedha kwa haraka kuwezesha kampuni za wazawa kufanya shughuli hiyo.

Naye mkazi wa mtaa wa Mirongo Leila Hassan amesema mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni ilikata baadhi ya kingo kwenye daraja la Nkrumah hivyo kuzua usumbufu na hofu kwa wananchi.

Hivi karibuni kufuatia mvua kubwa iliyonyesha madaraja ya Uhuru, Masai na Nkurumah yalibomolewa sehemu za kingo zake.

Wakati huo huo wakazi hao wa Jiji la Mwanza wamepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Jiji hilo za kubuni maeneo mazuri ya uwekezaji wa sekta mbalimbali zinazoweza kulipatia eneo hilo kipato cha kuchochea maendeleo ya watu wake.

Wameshuhudia miradi mingi ya kimkakati katika sekta za barabara , elimu, afya na miundombinu ikizidi kuendelezwa

Wamesema wanafarijika kuona kuwa ndani ya Jiji hilo baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hayajaendelezwa sasa yamefunguliwa kwa haraka ikiwemo eneo la ufukweni la Tampere.

Angelina Juma ambaye anajishughulisha na uuzaji wa bustani ya miti kwenye bustani ya Tampere amesema wamefurahi kuona eneo hilo likipimwa kwa ajili ya uwekezaji.

Wamepongeza ubunifu wa Mkurugenzi wa Jiji hilo Aroun Kagulumjuli kwa kutenga eneo la Tampere kwa ajili ya uwekezaji wa kuingizia mapato Jiji la Mwanza.

Pia Kagulumjuli ameweza kuweka msisitizo wa nidhamu kwa watumishi wa halmashauri hiyo kwani wanatenda kazi zao kwa haraka.