November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kuwahudumia wazee wasiojiweza

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbeya

`IMEELEZWA kuwa jamii imekuwa haina mwamko wa kuhudumia wazee katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya hali inayofanya kundi hilo kuendelea kuishi maisha duni na baadhi yao kutengwa na familia zao huku wengine wakiishia kulelewa kwenye vituo.

Kauli hiyo imetolewa Juni 3,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la The Livinghope Organization ambalo linajishughulisha na masuala ya wazee ,watoto na watu wenye ulemavu (TLHO)Lucy Mwakibete wakati akizungumza na Timesmajira jinsi taasisi hiyo inavyohudumia wazee wasiojiweza katika Wilaya ya Mbarali.

“Tumekuwa tukiendelea kupambana kutoa elimu kwa jamii kufahamu umuhimu wa kuhudumia wazee na kuwatunza pamoja na kuwaangalia kwani kipindi walipokuwa vijana wazee hawa walitumia nguvu zao nyingi kuwekeza kwa jamii,”amesema.

Akizungumza kuhusu baadhi ya wazee kutengwa na familia zao ,Mwakibete amesema wengi wao huhusishwa na imani za kishirikina kutokana na kufiwa na watoto wote hivyo kunyooshewa vidole na jamii kuwa anaua watoto wakati mwingine watoto hufariki kwa kuugua maradhi ya kawaida lakini si kurogwa.

“Tunajiandaa kutoa msaada wa chakula kwa wazee wetu wasiojiweza wa Kata ya Kongolo Mswiswi Wilaya ya Mbarali pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhudumia wazee sababu baadhi yao wamekuwa wakitelekezwa na kuishi maisha duni na wengine kuishi kwenye vituo vya kulelea wazee,”amesema Mwakibete.

Kwa upande wake Diwani wa Kata Igurusi , Hawa Kihwele amesema kuwa jamii kuwatenga wazee ni kukwepa majukumu na kuwa mikakati iliyopo ni kuendeleza mabaraza ya wazee ili kujua changamoto zao na wasiojiweza kabisa wanapewa pesa za TASAF.

Kihwele amesema kuwa jamii kuweka kigezo cha imani za kishirikina kwa wazee ni woga na elimu duni na kusahau kuwa wote ni lazima uzee uwakute kama kifo kikiwaacha na kuzeeka uchawi ni matishio ya jinsi ulivyo choka na uzee.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na Diwani wa Kata ya Itamboleo , Twalibu Lubandamo amesema kuwa ameona mabango mbalimbali ya wazee yakisema wazee ni dawa.

“Wengi wanaweza wasijue kwanini ni dawa nimeona migogoro mingi wanaharibiana vijana kwa vijana kwa maana wakiulizana changamoto hawawezi kupata majibu sababu akili zinafanana na umri,”.