Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Jamii imetakiwa kuungana kwa pamoja kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa lengo la kupambana na ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu huku wanawake wakitakiwa kuhakikisha wanajikita katika shughuli za kiuchumi na kuacha dhana ya kuwa tegemezi.
Pia Jamii imetakiwa kufichua siri za makundi ya wanawake wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao hatua ambayo imekuwa ikiwaathiri katika nyanja tofauti ikiwemo za kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na wanawake wanaofanya kazi katika bandari ya Tanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanayoadhimishwa duniani kote.
Akizungumza wakati akikabidhi misaada mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha nyumba ya furaha kilichopo eneo la Raskazone jijini Tanga Mkuu wa Idara ya rasilimali watu na utawala katika bandari ya Tanga Sharifa Nuhu amesema wapo baadhi ya kina mama wanashindwa kuelezea changamoto zinazowakabili katika familia zao hatua ambayo imekuwa ikiwaathiri katika nyanja tofauti ikiwemo za kiuchumi.
“Wanawake tunapaswa kuwa na uhuru wa kichumi wanaume wanapenda kunyanyasa wanawake ambao hawajitambui na hawana uwezo wa kichuni kwasababu anajua kabisa anategemea kila kitu kutoka kwa mwanaume hivyo atamfanya anachotaka nitoe rai kwa wanawake wenzangu tujitahidi kufanya kazi mbalimbali ambazo zitatuingizia kipato na kutuweka huru katika masuala yote ya kiuchumi kwenye zama hizi, “alisistiza Sharifa.
Kwa upande wake Katibu wa wanawake kutoka bandari ya Tanga Nancy Gerald amesema wanawake ni jeshi kubwa na lenye nguvu hivyo amewataka wanawake kupaza sauti zao pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili dhidi yao au kwa watoto kwani wanawake ndio wamebeba dhamana kubwa kwa Taifa ya kuwalea na kuwalinda watoto.
“Sisi wanawake tukikaa kimya hakuna chochote kitakachoweza kuendelea mabadiliko yaanzia kwa mama kwa kuwa mama ni mlezi hivyo upo uhitaji mkubwa wa wanawake wote watanzania kwenda kifua mbele tukiamini kwamba tunaweza kufanya mambo makubwa duniani kama anavyofanya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan, “alisema.
Mlezi na msimamizi wa kituo cha nyumba ya furaha, Sister Consolata Mgumba ameitaka jamii kujenga ukaribu na watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kwa sababu kituo chao kimekuwa kikilea watoto wanaotoka katika mazingira magumu na hatarishi wanayofanyiwa na walezi au jamii inayowazunguka.
“Sisi kama watawa wanawake tunawashukuru sana na msaada huu unatutia nguvu ya kuendelea kuwalea watoto hawa ambao wamepitia katika mazingira magumu ikiwemo ya kunyanyaswa jambo linalowaathiri watoto nyinyi mmetambua na mmeona kwamba mkileta msaada huu utatusaidia katika mahitaji mbalimbali nyinyi ni wanawake mnaoaminika na ni jeshi kubwa, “alisema Consolata.
Alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 70 huku mdogo kabisa akiwa na miezi 8 na mkubwa miaka 20.
Amesema ongezeko la watoto katika vituo vya kulelea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kunaashiria kwamba kuna kitu hakijakaa sawa hivyo ametoa wito kwamba jamii ione kila mtoto wa mwenzie ni mwanae na kumuhudumia popote anapokutwa hali itakayopelekea kupunguza ongezeko la watoto katika vituo vya kulelea.
“Sisi tunawajibika kufanya hiyo kazi lakini tukubaliane kwamba tunabeba maumivu ambayo jamii ingeweza kubeba kwani unapoletewa mtoto amefanyiwa ukatili uanze kumuhudumia cha kwanza wewe mwenyewe unaingia ule uwoga na maumivu unaumia pamoja na yeye lakini ikiwa tutasimama pamoja tutaungana ukatili huu utapungua na ikiwezekana utaisha kabisa na hizi makao za kulele zikaisha kabisa, “alisisitiza.
Aliongeza kuwa nina ushuhuda kuna makao kule nje ya nchi hii zaman kule Ulaya tulikuwa na vituo 52 na leo ninavyoongea Ulaya tuna vituo vitatu tuu kwakuwa imeruhusiwa kuwachukua watoto jamii inapaswa kujua watoto wanapolelewa kwenye makundi inawaathiri sana kisaikolojia kutokana na kulelewa katika mazingira tofauti na watu tofauti, “alisema Consolata.
Msaada huo ni pamoja na magodoro 20, vyakula , mavazi, madaftari ya shule, soksi, taulo za kike na kwamba wamefanya hivyo ikiwa nisehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika machi 8 kila mwaka.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu