December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kutazama wenye ulemavu kwa jicho la huruma

Na Esther Macha,Timesmajira Ontime. Mbeya

JAMII imetakiwa kuwatazama walemavu kwa jicho la huruma na kuhakikisha, inawawekea mazingira rafiki yatakayowawezesha kujikinga kwa urahisi na maambukizi ya Virusi vya Corona (Covid-19).

Kwa mujibu wa Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) Mkoa wa Mbeya, bado mazingira na miundombinu ya kujikinga na Covid-19 imewekezwa zaidi kwa watu walio na ukamilifu wa viungo na kuwaacha katika wakati mgumu walemevu.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CHAWATA mkoani hapa, Jimmy Ambilikile wakati akizungumza na Majira ambapo alisema, kati ya maeneo ambayo walemavu wamesahaulika kwa miundombinu ya kujikinga ni pamoja na maeneo ya taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa jamii.

Ambilikile amesema yapo baadhi ya maeneo, mlemavu anapofika analazimishwa kunawa mikono yake kabla ya kupewa huduma, jambo ambalo ni sahihi lakini changamoto inayokuja ni pale chombo cha kunawia kinapokuwa katika kimo asichoweza kufikia na hakuna njia mbadala anayoweza kuitumia kunawa.

Amesema pia kwa walemavu wanaotumia fimbo au baiskeli mwendo, wanakabiliwa na changamoto zaidi kwa kuwa kimsingi hawapaswi kuishia kutakasa mikono pekee kama inavyotafsiriwa na wanajamii wengi, bali hata vifaa hivyo wanavyotumia vinapaswa pia kutakaswa.

“Mlemevu mwenyewe unahitaji kujikinga na Corona, anayekusindikiza naye anahitaji, bado kama unatumia fimbo au baiskeli lazima navyo uvikinge ili visibaki na vijidudu. Sasa unaweza kuona mazingira ya walemavu yalivyo magumu.

“Lakini pia wapo walemavu wanaotambaa au wasioona, hawa lazima mazingira ya kujikinga kwenye maeneo ya kupata huduma yawe tofauti,” amesema.

Ameongeza: “Tumeona wadau wengi wakijitolea kutoa misaada kwa serikali. Wametoa vitakasa mikono lakini tunaona serikali inavisambaza kwa ujumla kama vile watu wake wote tuko sawa…kumbe ilipaswa pia kuwatizama watu walio na mahitaji maalumu ili wasibaki nyuma katika mapambano haya,” alisisitiza.

Mwenyekiti huyo amesema, bado kuna changamoto kwa walemavu wanaojishughulisha na ujasiriamali kwa kuwa utekelezaji wa kuhakikisha maeneo yao yanakuwa na vitakasa mikono ikiwemo maji yanayotiririka ni mgumu kwa kuwa, hawana uwezo wa kubeba maji kutoka yanakopatikana hadi maeneo ya shughuli zao kutokana na asili ya baadhi yao.