January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kutambua mchango wa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto yatima

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

WAMILIKI wa Vituo vya kulelea watoto yatima wameitaka jamii kuelewa kazi wanayoifanya kwa ajili ya watoto hao na siyo kuwanyooeshea vidole kwamba wamiliki hao wanapokea fedha nyingi jambo walilosema siyo kweli.

Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Mmiliki wa Kituo cha Watoto Yatima cha Sifa Kilichopo Kata ya Pangani Mkoa wa Pwani Sifa John wakati akizungumza na mwandishi wa habari.

Amesema watu wengi wamekuwa wakidhani kuwa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto yatima wanapata mabunda ya fedha kutoka kwa wafadhiri jambo alilosema kuwa siyo kweli badala yake wamiliki hao wamekuwa wakipitia changamoto kubwa zikiwemo za upungufu wa chakula cha kuwalisha watoto hao.

“Naomba niseme ukweli kwamba umefika wakati kwamba jamii ituelewe kwamba tunapitia kwenye changamoto kubwa wakati tukiwahudumia watoto hawa…..hivi unajua ugumu uliopo wakati ukimlea mtoto wa mwanamke mwenzio ????? Alihoji.

“Hivyo basi jamii itupe ushirikiano ili watoto hawa waweze kukua katika maadili mazuri kama wenzao wanaolelewa na wazazi wao wenyewe lakini pia niiombe Serikali ituamini kwamba kwa hili tunalolifanya na kujua kwamba tunapitia katika wakati mgumu,”

Mwanzilishi wa Taasisi ya vijana wanafunzi inayojulikana kama Young Investors Association (YIA) iliyofika kituoni hapo kwa ajili ya kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto hao zaidi ya 56 ilisema ni wajibu wa kila kijana na jamii mzima kwa ujumla kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto hao.

Mwanzilishi wa Taasisi hiyo ya YIA Joseph Mramba mara baada ya kukabidhi msaada huo, amesema yeye pamoja na wanafunzi wenzake waliona umuhimu wa kutoa msaada huo kidogo kwa ajili ya watoto na kusema kuwa hawataishia hapo badala yake watawafikia watoto wengi zaidi Nchini.

Amesema pia ni wakati muhafaka kwa wadau na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto wenye uhitaji wa mahitaji mbalimbali (yatima) ikiwemo chakula na malazi kwa madai kuwa kufanya hivyo kutawaondolea upweke watoto waliopo kwenye vituo vya kulelewa.

Mara baada ya kukabidhi msaada huo amesema “unajua sisi bado ni vijana ambao ni Taifa la leo na kesho hivyo tumeona upo umuhimu wa kushirikiana na watoto hawa katika kuhakikisha tunawapa faraja kwa kutoa misaada kidogo kama unavyoona,”.

Aidha amesema kuwa msaada mwingine kupitia Taasisi yake pamoja na wanafunzi wenzake watahakikisha wanawalipia bima watoto wawili wakati wakiendelea kujikusanya ili waweze kuwafikia watoto wengi zaidi waliopo katika kituo hicho na vituo vingine.

Katibu wa Kituo hicho cha kulelea watoto cha Sifa Erick Nakashange, alisema kuwa kituo chake kinakabiliwa na changamoto nyingi lakini kubwa zikiwa ni zile za uhaba wa chakula.

Amesema kuwa changamoto nyingine ni pamoja na baadhi ya watoto kutembea umbali mrefu, eneo la kituo kutokuwa na uzio pamoja na baadhi ya wanafunzi kutokuwa na bima za afya.

“Tunaiomba Serikali kuwa na bima za upendeleo hasa kwa hawa watoto ili iweze kutupunguzia mzigo na hasa pale watoto wanapougua,” amesema Nakashange.

Naye Katibu kutoka Taasisi ya YIA Hadiya Balozi, amesema kuwa wameguswa na kuona kwamba kuna umuhimu wa kuchangishana na wanafunzi wenzao ili waweze kuwasaidia watoto hao.

“Nipende kusema kuwa hawa bado ni watoto hivyo basi sisi dada zao lazima tuwatembelee, tuzungumze nao na kuwapa moyo ili siku za usoni wasije kukata tamaa,” amesema Katibu huyo.

Hata hivyo amesema kuwa ni wakati muhafaka kwa taasisi, serikali, wadau na jamii kwa ujumla kuona umuhimu wa kujitokeza na kushirikiana na watoto yatima.