Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
ILI kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu wanapata elimu jamii imeaswa kutowaficha ndani watoto wenye mahitaji tofauti ya kujifunzia ambayo hawawezi kuchangamana na watoto wenzao kila wakati kwani hivi sasa kuna mwongozo maalum wa shule ya nyumbani ambayo inawafikia watoto wote wenye changamoto hiyo.
Akizungumza na waandishi habari leo Septemba 11,2024 wakati wa uzinduzi wa mradi wa SAUTI ZETU unaolenga elimu jumuishi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo kuwa la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya watoto wenye ulemavu (CST),Noela Msuya amesema kuwa jamii ihakikishe kuwa hakuna mtoto anayebaki nyumbani kwa kisingizio cha ulemavu au changamoto yeyote inayotokana na ulemavu.
“Sasa hivi elimu yetu imekuwa na mfumo wa elimu jumuishi lakini tuna sera na mikakati mizuri ya elimu hata kwa watoto wanaobaki nyumbani ambaye anamahitaji tofauti ya kujifunza akitolea mfano watoto wenye magonjwa ambayo hawawezi kuchangamana na watoto wenzao kila wakati sasa hivi nchi yetu ina mwongozo wa shule ya nyumbani ambapo watoto wanafikiwa na kufundishwa kwa ufasaha hivyo tusifiche watoto ndani hata kama wanaumwa taarifa zitolewe kwa maafisa elimu ili watafutiwe walimu ambao watatumia mwongozo wa shule ya nyumbani “amesema Msuya.
Akielezea kuhusu mradi wa SAUTI ZETU Msuya amesema kuwa wameandaa kwa kushirikiana na Haki elimu na wadau wengine na kwamba kuna mashirika sita katika kulenga ufuatiliaji utekelezaji wa mpango mkakati wa elimu jumuishi na katika mradi huo wanategemea kuangalia jinsi elimu jumuishi ilivyofikiwa pamoja na changamoto zake na kama wananchi wanaelewa mpango mkakati na miongozo yake kama ipo kwenye maeneo husika mfano shule pamoja na maafisa elimu,maafisa maendeleo ya jamii.
Hata hivyo Msuya amesema kuwa kwenye mradi huo wanaenda kukusanya taarifa ambazo zitasaidia kuonyesha katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji ya mpango mkakati wa elimu jumuishi wameweza kufikia malengo yao kwa kiasi gani .
“Leo tulikuwa na uzinduzi ambapo tumeleta wadau muhimu ambao wote wana lengo moja katika utekelezaji wa elimu jumuishi lakini pia katika masuala ya ulinzi na usalama wa watoto ,katika uzinduzi huu tumewaleta maafisa elimu, maafisa ustawi wa jamii ,vyama vya watu wenye ulemavu sababu hatuwezi kufanya shughuli yeyote bila wao wenyewe kuwepo wote hawa ni wadau muhimu katika kufanya ufuatiliaji na utekelezaji wa mipango mkakati mbali mbali inayohusu watoto wenye ulemavu”amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa Mbeya ,Salum Mayendi amesema kikao kazi kilichoitishwa na Chid support Tanzania kina manufaa makubwa kwa wataalam ambao wanatekeleza huduma za ustawi wa jamii katika mkoa wa Mbeya ambapo wahusika wakuu walikuwa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu na wadau wengine kwa kujifunza miongozo ambayo inahusisha elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu hususani watoto .
“Lakini huwezi kuichukua elimu bila kuweka ulinzi na usalama wa watoto kwani hivi sasa kuna matukio mengi ya watoto kufanyiwa ukatili na vitendo vya ubakaji na ulawiti kupitia kikao hichi tumejifunza ulinzi na usalama wa mtoto kimsingi tumeweza kugundua kuwa serikali imeweka mwongozo na sera mbali mbali za kutekeleza elimu jumuishi ,tumeweka mikakati na kusambaza mwongozo na kumfikia mtu wa chini na muhusika anayelengwa na wataalam wanaotekeleza huduma kwa watu wenye ulemavu ,viongozi na kutoaliacha kundi hili wakati wa kutekeleza maendeleo ya Taifa letu hatuwezi kuwaacha watu wenye ulemavu”amesema Mayendi.
Mkazi wa Kabwe Jijini Mbeya , Prosper Ayub amesema kuwa katika jamii bado kuna changamoto ya ufahamu wa elimu jumuishi na kusema ipo haja kwa serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kupata ufahamu kwani baadhi ya watu bado uelewa wao ni mdogo .
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria