November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yaaswa kusaidia watoto yatima kutimiza ndoto zao

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAZAZI, walezi, taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo wameshauriwa kusaidia watoto wanaotoka katika familia maskini na yatima ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao ikiwemo kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 25 ya Huduma ya Maendeleo ya Mtoto na Kijana iliyofanyika juzi Kitaifa katika uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui Mkoani hapa.

Amesema kuwa watoto wengi wanaotoka katika familia duni na wale walioachwa yatima kutokana na kuondokewa na mmoja wa wazazi wao au wazazi wote wamekuwa wakipoteza mwelekeo wa maisha kwa kukosa watu wa kuwasaidia.

Amebainisha kuwa watoto wana vipaji vingi na ndiyo Viongozi wa kesho, hivyo kama wazazi, walezi, taasisi na wadau mbalimbali wataamua kuwekeza kwa watoto na kuwasaidia wale wote wasio na uwezo, kesho yao itakuwa bora zaidi.

Naibu Waziri amelipongeza Shirika la Compassion International Tanzania (CIT) kwa kutimiza miaka 25 tangu lianze kutoa huduma ya kusaidia watoto yatima na wanaotoka katika familia duni katika Mikoa mbalimbali hapa nchini.

‘Nawapongeza sana Shirika la CIT kwa mchango mkubwa mliotoa na mnaoendelea kutoa kwa watoto na vijana wasiojiweza kwa kuwapatia elimu na ujuzi wa fani mbalimbali na kusaidia familia zao kujikwamua kiuchumi’, ameeleza.

Amesisitiza kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakitumia fedha nyingi sana kwenye harusi na starehe nyinginezo wakati kuna watoto jirani yao ambao wana uhitaji mkubwa wa elimu na hawana mtu wa kuwasaidia.

‘Kutoa msaada wa kielimu, chakula au mahitaji mengine ya aina yoyote ile kwa watoto yatima ni sadaka nzuri sana tena inayompendeza Mungu kuliko kuchangia mamilioni kwenye harusi ili watu wakale na kunywa bia, tutafakari upya’, amesema.

Dkt Mollel ametoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kusaidia watu wasiojiweza ili kutoa sadaka iliyo njema machoni pa Mungu kwa kuwa yeye ndiye alitoa kila kitu tulicho nacho hapa duniani, kutoa ni kurudisha shukrani kwa Mungu.

Amemba Viongozi wa Shirika hilo, Maaskofu na Wachungaji ambao ndio walezi wa Vituo vya Kulelea Watoto hao kuendelea kuwalea vizuri ili wakue katika maadili mema na kuwa viongozi wazuri kwa jamii hapo baadae.

Awali Mkurugenzi wa Shirika hilo Mary Lema amemweleza Naibu Waziri kuwa Shirika hilo lilioanza hapa nchini mwaka 1999 limekuwa moja kati ya Mashirika makubwa ya Kikristo ya maendeleo hapa nchini.

Amesema kuwa hadi sasa wanafanya kazi na Makanisa zaidi ya 550 ambayo ndiyo Washirika wenza na wapo katika Mikoa 21 ya Tanzania Bara kwenye halmashauri zaidi ya 80, na watoto zaidi ya laki 115 kutoka katika wilaya hizo wanafadhiliwa.

Ameongeza kuwa tangu kuanza huduma hiyo wamefanya mambo mengi ikiwemo kusaidia kaya maskini zaidi ya laki 2, kuanzisha shule za awali na msingi zaidi ya 300, watoto zaidi ya 39,000 wamepewa elimu ya sekondari na ujuzi, vijana zaidi ya 65,000 wamehitimu mafunzo ya kozi mbalimbali na vijana zaidi ya 32,500 wamepata elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu.