April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jafo aipongeza iTrust Finance kudhamini Soko la Jiba Souk

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WADAU na wafanyabiashara nchini wametakiwa kujitokeza na kuiga mfano wa kampuni ya huduma za kifedha nchini, iTrust Finance Limited kwa kudhamini jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na masoko ya bidhaa za wafanyabiashara wadogo na wa kati hususani wanawake.

Rai hiyo imetolewa leo jioni na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, wakati alipotembelea maonesho makubwa ya Soko la Jiba Souk yaliyofanyika katika Viwanja vya Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam yakiwaleta pamoja wajasiriamali wadogo zaidi ya 250  na kuvutia  watu zaidi ya 13,000.

Waziri Jafo ameipongeza iTrust kwa kushirikina na wajasiriamali hao kama mdhamini mkuu katika tukio hilo muhimu lenye lengo la kukuza fursa za biashara na uchumi miongoni mwa wanachama wake pamoja na Watanzania kwa ujumla.

Kwa mujibu wa iTrust Finance, udhamini huu ni sehemu ya dhamira yake ya kukuza uhuru wa kifedha kwa kuunda fursa za maendeleo endelevu. 

Kampuni hiyo inalenga kusaidia biashara zinazoongozwa na wanawake, huku ikifungua milango ya uthabiti wao wa kifedha kwa siku zijazo.

“Fedha zetu za uwekezaji zitawasaidia wajasiriamali hawa kuweka akiba kwa ajili ya elimu ya watoto wao, kuhakikisha mustakabali wao, na kufanikisha mpango wa kustaafu kwa amani,” ilieleza taarifa kutoka iTrust Finance.

Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance, Faiz Arab, alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kufanikisha ujumuishaji wa kifedha kwa wamiliki wa biashara ndogo. 

“Kama kampuni ya huduma za kifedha inayojitolea kwa ujumuishaji na uwezeshaji wa kiuchumi, tunaona udhamini huu kama hatua muhimu ya kuziba pengo la kifedha na kuimarisha ustawi wa muda mrefu wa wafanyabiashara wadogo,” alisema Faiz.

Kupitia mpango huo, iTrust Finance inatarajia kuangazia matokeo chanya ya mafanikio ya wajasiriamali wanawake na kuonesha jinsi uwezeshaji wa kifedha unavyoweza kubadili maisha yao. 

“Juhudi hizi ni sehemu ya mpango wa iTrust W.I.S.E (Women in Investments and Securities Education), ambao unalenga kujenga jamii ya wanawake walioelimika kifedha na wenye nguvu katika kushiriki fursa za uwekezaji.” Aliongeza Faiz.

Kampuni hiyo inawaalika wananchi kushiriki na kushuhudia matokeo ya ushirikiano huu, huku wakisherehekea maendeleo ya biashara zinazoongozwa na wanawake nchini Tanzania.

JIBA Dar es Salaam, ambayo ni mwenyeji wa Soko la Jiba Souk, ni sehemu ya JIBA International shirika lililoanzishwa mwaka 1991 kwa lengo la kukuza fursa za biashara na uchumi miongoni mwa wanachama wake, hasa kutoka jamii ya kimataifa ya Khoja Shia Ithna-Asheri.