November 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JAB yahimiza habari za kina kuhusu nishati safi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuandaa habari za kina zinazoibua changamoto halisi zinazowakabili wananchi katika kuanza na kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia, ili kuchochea upatikanaji wa suluhisho na kufanikisha malengo ya kitaifa.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 13, 2026, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Nishati Safi ya Kupikia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DAR-PC), jijini Dar es Salaam.

Wakili Kipangula amependekeza kila chombo cha habari kuandaa angalau habari moja ya kina inayojibu changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo gharama za kuanza kutumia nishati safi, usalama wa vifaa, upatikanaji wake, changamoto za usambazaji, uzoefu wa watumiaji pamoja na fursa za biashara na uwekezaji.

“Habari tunazotoa zinapaswa kujibu maswali ya wananchi na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi. Ni muhimu kuwaelimisha kuhusu gharama za matumizi, usalama wa vifaa na upatikanaji wa nishati safi katika maeneo yao,” amesema Wakili Kipangula.

Amesema Waandishi wa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, rahisi kueleweka na zinazozingatia mazingira yao kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa habari zinazobeba uzoefu wa wananchi na ushahidi wa kutosha zinaweza kuisaidia Serikali pamoja na wadau wengine kutambua mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Aidha, Wakili Kipangula amewataka Waandishi wa Habari kuzingatia ukweli, takwimu sahihi na maadili ya taaluma wanaporipoti masuala ya nishati safi, akisisitiza kuwa kasi ya kutoa taarifa haipaswi kupewa nafasi kuliko usahihi wake.

“Habari ya kwanza si bora kama si sahihi. Mwandishi wa Habari mwenye weledi si yule anayewahi kutoa taarifa pekee, bali ni yule anayehakikisha taarifa anayotoa ni ya kweli, imehakikiwa na ina manufaa kwa jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DAR-PC, Bakari Kimwanga, ameeleza mafanikio ya klabu hiyo, yakiwemo kuongezeka kwa idadi ya wanachama, Waandishi wa Habari kuendelea kujiendeleza kielimu na kuimarika kwa ushirikiano na maafisa pamoja na wadau mbalimbali katika upatikanaji wa taarifa.

Mkutano huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Nishati Safi ya Kupikia kwa Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa 2050,” ukiwakutanisha Waandishi wa Habari, wataalamu, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa sekta ya nishati.