May 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Itunda aipongeza Mbeya ukusanyaji mapato

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbeya imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 104 katika mwaka wa fedha uliopita, hatua ambayo imepongezwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Solomon Itunda.

Itunda amesema mafanikio hayo yanaonyesha usimamizi mzuri wa rasilimali za halmashauri pamoja na uwajibikaji wa watendaji katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Amesema mafanikio hayo yametokana na nidhamu ya kazi, ubunifu na mshikamano miongoni mwa watumishi wa halmashauri, hali iliyosaidia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

“Mafanikio haya yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi katika kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi,” amesema Itunda.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo na ukusanyaji wa mapato kilichofanyika wilayani humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Erica E. Yegella, amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato pamoja na ushirikiano mzuri kati ya watumishi na wadau wa maendeleo.

Yegella amesema menejimenti ya halmashauri itaendelea kusimamia kwa weledi ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi wa wilaya ya Mbeya.