Na Jumbe Ismailly,TimesMajira Online
SUALA la lishe ni suala mtambuka na limepewa kipaumbele katika Mkoa wa Singida na Mkoa utaendelea kuhakikisha kwamba fedha zilizotengwa zinatumika kutekeleza afua za lishe zenye kuleta matokeo chanya katika jamii.
Bajeti ya kutekeleza shughuli za lishe katika Halmashauri za Mkoa wa Singida imeongezeka kutoka sh. 115,697,932 kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 mpaka kufikia sh. 342,823,103 kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 sawa na shilingi 1,239 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano.
Mkoa wa Singida utahakikisha fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kutekeleza shughuli za lishe kama zilivyopangwa na utaendelea kuhamasisha Halmahauri kutenga fedha za lishe kulingana na mwongozo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kutekeleza shughuli zilizopangwa.
Mkoa wa Singida una jumla ya wakazi 1,705,180 ambao kati yao, watoto chini ya miaka mitano ni 276,590 huku kukiwa na jumla ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wapatao 395,814.
Mkoa wa Singida una jumla ya Halmashauri saba ambazo ni pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Singida,Halmashauri ya wilaya ya Singida,Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Halmashauri ya wilaya ya Iramba,Halmashauri ya wilaya ya Mkalama na Halmashauri ya Itigi.
Mkoa wa Singida una jumla ya vituo 245 vya kutolea huduma za afya,ikiwa na Hospitali 11,vituo vya Afya 20,zahanati 210 pamoja na Kliniki 4.
Aidha kati ya vituo vya afya 245 vilivyopo,vituo 99 vya kutolea huduma za Afya vinatoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa wagonjwa wa ndani na nje ya Mkoa wa Singida.
Katika Makala haya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba,Dkt. Hussein Sepoko anazungumzia hali ya ujenzi wa jengo la tiba ya lishe lililopo katika Hopitali ya wilaya ya Iramba,litakavyosaidia kutambua viashiria vya lishe pamoja na vipaumbele katika kuhakikisha lishe duni inapungua kama siyo kumalizika kabisa.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wiaya ya Iramba,Dkt.Hussein Sepoko anasema Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imejenga jengo la kutolea huduma za tiba kwa njia ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano,walio na changamoto ya utapiamlo mkali na usio mkali.
Anafafanua Dkt.Sepoko kuwa jengo hilo limejengwa kwa udhamini mkubwa wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la ACTION AGAINST HUNGER ambalo ndilo lililotoa gharama zote za ujenzi pamoja na vifaa tiba.
Aidha anasema jengo hilo limetumia jumla ya sh.111,798,320 ikiwa ni gharama za ujenzi na shilingi 11,470,000/= zikiwa ni gharama za samani za jengo zima vikiwemo vitanda, meza,kabati,viti,vifaa tiba mbali mbali vitakavyotutumika kuandalia vyakula lishe wakati wa utoaji wa tiba kwa watoto.
Anasema jengo hilo kwa sasa limekamilika kwa ajili ya matumizi ya kutoa tiba kwa watoto wote wanaogundulika kuwa wana utapiamlo mkali na usio mkali na litatumika kama rufaa kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya za Halmashauri ya wilaya ya Iramba pamoja na vya majirani.
“Jengo hili lilianza kujengwa tarehe 18/09/2020 na kukamilika tarehe 20/05/2021na kwa sasa jengo hili limeanza kutoa huduma kwa watoto wanaogundulika kuwa na utapiamlo”anasisitiza Mganga mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo Dkt.Sepoko anazitaja changamoto zilizojitokeza wakati wa ujenzi wa jengo hilo kuwa ni pamoja na upungufu wa chakula dawa (F100) na RUTF (PLUMPY NUTS) ambazo ndizo zina matumizi zaidi.
“Changamoto kubwa ambayo ipo kwa sasa ni upungufu wa chakula dawa (F100) na RUTF (PLUMPY NUTS) ambazo ndizo zina matumizi zaidi”anafafanua zaidi Dkt Sepoko.
Mganga mkuu huyo hata hivyo anazitaja faida za jengo hilo pindi litakapokamilika kuwa ni kuwawezesha watoto waliobainika na changamoto za utapiamlo kupata huduma bora zinazostahili na kupunguza changamoto kubwa ya utapiamlo kwa watoto kutokana na tiba pamoja na elimu mbali mbali zitakazokuwa zinatolewa katika jengo hilo.
Faida zingine ni kuwawezesha watoto kupata huduma katika mazingira rafiki kutokana na changamoto zinazowakabili pamoja na jengo hilo litatumika kama kitengo cha rufaa kwa watoto wenye changamoto ya utapiamlo kutoka katika Halmashauri zingine zilizopo ndani ya Mkoa wa Singida.
“Tunaishukuru serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la ACTION AGAINST HUNGER kwa kuweza kutujengea jengo la tiba ya lishe katika Halmashauri yetu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ili kutoa tiba kwa watoto hao na pia kupunguza utapiamlo kwa ujumla”anasisitiza Dkt Sepoko.
Akizindua jengo la lishe lililojengwa kwa ufadhili wa Gross Foundation & M-CIAD kupitia Shirika la Action Against Hunger Tanzania,Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Godwin Mollel amewaagiza wataalamu wa idara ya kinga katika wizara hiyo kuangalia uwezekano wa kutumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu masuala ya afya badala ya kutumia machapisho ili kupunuza gharama.
Aidha Naibu Waziri Mollel anasema idadi ya watu wanaosoma machapisho ni wachache sana,lakini ukiangalia gharama za machapisho ni kubwa sana ukilinganisha na gharama za kutangaza kwenye vvyombo vya habari.
Hata hivyo Naibu waziri huyo anasema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa wataalamu wa idara ya kinga katika wizara hiyo kuona umuhimu wa kupunguza machapisho ili fedha ambazo zingetumika kuchapisha machapisho ya shilingi milioni kumi wanaweza kutumia shilingi milioni mbili tu kwa kupeleka kwenye tasnia ya habari na ujumbe huo ukawa umefikia wananchi na wakawa wameokoa shilingi milioni nane.
“Nikafikiri kuna umuhimu wa kupunguza machapisho ili fedha hizo sehemu ambazo ungechapisha machapisho ya shilingi milioni kumi unaweza ukatumia tu shilingi milioni mbili ukapeleka kwenye tasnia ya habari ule ujumbe ukawa umewafikia wananchi ukawa umeokoa milioni nane na hiyo milioni nane inakuja kwa watoto wenye utapiamlo kama hawa”anafafanua.
Aidha Mollel hata hivyo anasisitiza kwamba wamejifunza kwenye magonjwa mengi yamepitishwa zaidi na vyombo vya habari,lakini pia akatumia fursa hiyo kuwaomba waandishi wa habari waliopo serikalini kujiongeza.
“Lakini tunawaomba watu wa idara ya kinga kwenye wizara ya afya wajiongeze kwani unapozungumza upo kwenye idara ya kinga ni tasnia kubwa unapokuwa kiongozi wa idara ya afya siyo kuokota ile miongozo na jinsi serikalini ilivyozoeleka,chapisha sijui nenda mwenyewe kwenye tv ongea,hapana ni kwamba unaunganisha na wizara ya habari unashirikina na wizara zingine na waandishi wa habari halafu unahakikisha ujumbe wako umefika kwa lugha rahisi na njia nyepesi.”anasisitiza Naibu waziri huyo.
Mratibu wa mradi wa Action Against Hunger,Lydia Mshengezi anabainisha kwamba Shirika hilo la kimataifa ambalo si la kiserikali na ambalo limejikita zaidi katika kupigana na njaa pamoja na madhara yatokanayo na njaa.
Kwa mujibu wa mratibu huyo wa mradi kwa mara ya kwanza Tanzania ilipata ufadhili mwaka 2015 na baada ya hapo wakawa wamepata nafasi ya kuweza kushiriki katika mikakati mbali mbali serikalini ikiwemo kuandaa mkakati wa lishe kitaifa wa mwaka 2016-2021
Mratibu wa Lishe Mkoa wa Singida,Teda Sinda anaelezea hali ya lishe,mwelekeo wa hali ya lishe kwa watoto,mwelekeo wa viashiria vya lishe pamoja na vipaumbele vya Mkoa wa Singida katika kuhakikisha lishe duni inapungua kama siyo kumalizika kabisa.
Teda anasema lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na tatizo hili ni moja ya chanzo kikubwa cha vifo vya watoto wadogo, ingawa ni mara chache tatizo hili hutajwa kama sababu ya moja kwa moja iliyosababisha kifo.
Anasema lishe duni pia hudumaza ukuaji wa watoto kimwili na kiakili hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri mashuleni na pia hupunguza ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima na ndio maana msisitizo mkubwa unawekwa katika kuwekeza lishe bora ndani ya siku 1,000 za mwanzo za mtoto,yaani kuanzia mimba inapotungwa mpaka mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili ili kuondokana na tatizo hili la udumavu.
Aidha Mratibu huyo anasema mbali na tatizo la lishe kwa watoto, takwimu zinaonyesha kwamba katika Mkoa wa Singida, mwanamke mmoja kati ya kumi ana ukondefu na tatizo hilo hupelekea wanawake hao wenye lishe pungufu kuwa katika hatari ya kupoteza maisha pindi wanapojifungua kwa kupungukiwa damu,kujifungua watoto wenye uzito pungufu,hali hii husababisha urithishaji wa hali duni ya lishe kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Anasema Teda kuwa Mkoa unaendelea kuhakikisha shughuli za lishe zinatekelezwa katika Halmashauri zote kwa kufuata sera na miongozo ya Wizara ya Afya ambapo kila Halmashauri ina Mratibu wa lishe ambaye amejengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
Pia anasema kila Halmashauri ina kamati ya lishe ambayo ina jukumu la kusimamia shughuli za lishe katika sekta zote mtambuka za lishe,ikiwemo sekta ya kilimo,sekta ya maendeleo ya jamii,sekta ya maendeleo ya mifugo pamoja na sekta ya mipango.
Hata hivyo mratibu huyo wa lishe Mkoa wa Singida anafafanua kuwa wadau mbali mbali wamekuwa wakitekeleza shughuli za lishe katika Mkoa wa Singida,wakiwemo Action Against Hunger wamekuwa wakitekeleza mradi wa lishe imara katika Halmashauri tatu ikiwemo Halmshauri ya wilaya ya Mkalama,Halmashauri ya wilaya ya Iramba na Halmashauri ya Itigi.
Kwa mujibu wa mratibu huyo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na SEMA pamoja na RECODA wamekuwa wakitekeleza mradi wa Boresha Lishe katika Halmashauri mbili za Ikungi pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Singida.
Hata hivyo Mratibu huyo anasema kwamba Shirika la World Vision Tanzania wamekuwa wakitekeleza mradi wa ENRICH katika Halmashauri ya wilaya ya Ikungi na Halmashauri ya wilaya ya Manyoni na kwamba mradi wa Boresha lishe umemalizika na tayari umeshakabidhiwa katika ngazi ya Mkoa.
Kuhusu hali ya lishe katika Mkoa wa Singida,mratibu huyo anaweka wazi kuwa kutokana na utafiti wa lishe kitaifa (TNNS) wa mwaka 2018 umeonyesha kwamba hali ya lishe ya watoto chini ya miaka mitano Mkoani Singida imefikia asilimia 29.8 na kuwa watoto chini ya miaka mitano wana udumavu.
Aidha utafiti huo pia umebaini kwamba asilimia tano ya watoto chini ya miaka mitano wana ukondefu,wakati asilimia 15 ya watoto chini ya miaka mitano wana uzito mdogo,asilimia 11 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 wana ukondefu na asilimia 6.1 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wana uzito mkubwa.
Kadhalika anasisitiza kuwa asilimia 17 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wana upungufu wa damu wakati watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita(Exclusive breastfeeding) ni asilimia 57.7,wakati asilimia 27.9 ni ya watoto walionyonya maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili pamoja na watoto chini ya miaka miwili ambao hupata walau mlo unaokubalika kilishe ni asilimia tatu.
Mratibu huyo wa lishe Mkoa wa Singida anasema mwelekeo wa hali ya lishe kwa watoto (TNNS 2014 VS TNNS 2018) unaonyesha kwamba kwa mwaka 2014 watoto wenye aina ya utapiamlo wenye udumavu ni asilimia 34 wakati wenye ukondefu ni asilimia 4.7 na wenye uzito mdogo ni asilimia 15.
Kwa mwaka 2018,Teda anasema kwamba watoto wenye aina ya utapiamlo wenye udumavu ni asilimia 29 wakati wenye ukondefu ni asilimia 5.2 na wenye uzito mdogo ni asilimia 14.
Akizungumzia mwelekeo wa viashiria vya lishe katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi,2020 na mwaka 2021,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dkt.Victorina Ludovick anasema watoto walio na uzito pungufu kwa mwaka 2020 kwa watoto wenye umri wa miezi 0 – 59 ni asilimia 3.3 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2021 ni asilimia 5.9.
Dkt Victorina anasema kuwa watoto wenye udumavu wenye umri wa miezi 0- 59 ni asilimia 0.16 kwa mwaka 2020 wakati kwa mwaka 2021 ni asilimia 0.16,wakati watoto walio na ukondefu ni asilimia 0.28 kwa mwaka 2020 na asilimia 0.31 kwa mwaka 2021,watoto waliozaliwa na uzito pungufu chini ya uzito wa kilo 2.5 ni asilimia 4.3 kwa mwaka 2020 na asilimia 5.1 kwa mwaka 2021.
Mganga mkuu huyo hata hivyo anasema kwa wanawake wajawazito waliokutwa na upungufu wa damu katika hudhurio la kwanza ni asilimia 1.4 kwa mwaka 2020 na asilimia 1.8 kwa mwaka 2021,watoto walionyonya maziwa ya mama ndani ya lisaa limoja ni asilimia 96 kwa mwaka 2020 na asilimia 92 kwa mwaka 2021 na kwa wajawazito waliopewa vidonge vya kuongeza damu ni silimia 72 kwa mwaka 2020 na asilimia 73 kwa mwaka 2021.
Aidha dkt Victorina anasema takwimu zinaonyesha tatizo la udumavu limepungua kwa hali inayoridhisha ukilinganisha na matatizo mengine ya kilishe lakini bado changamoto kubwa ipo kwenye uzito mdogo na ukondefu na kikubwa kinachochangia matatizo haya ni ulishaji duni kwani kuna tabia ya wanawake wengi kwenda kujitafutia vipato na kuwaacha watoto wakilelewa na watu wengine hususani bibi zao.
Anasisitiza Mganga mkuu huyo kwamba juhudi mbali mbali zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha tatizo la utapiamlo linapungua kabisa katika Mkoa wa Singida kwa kuendelea kuainisha maeneo hasa yaliyo na watoto wengi wenye ukondefu katika jamii ikiwa ni pamoja na kushirikisha wadau mbali mbali wa lishe kufanya utafiti wa kina kujua.
Mikakati mingine kwa mujibu wa Mganga mkuu huyo ni kutoa elimu ya ulishaji na unyonyeshaji wa watoto wachanga na wadogo ikiwa ni pamoja na kushirikiana kutoa elimu ya malezi hasa kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi na kutumia majukwaa mbali mbali kutoa ujumbe lishe ikiwa ni pamoja na kutumia redio Standard ya Singida kuongea na na jamii kuhusiana na masuala ya lishe.
Mingine ni kuwajengea uwezo watoa huduma ngazi ya kituo na ngazi ya jamii kuhusiana na utoaji wa huduma za lishe katika maeneo yao,kuzijengea uwezo kamati za lishe za Halmashauri ili ziweze kufanyakazi kwa ufanisi katika kutokomeza tatizo la utapiamlo kwa kuzingatia majukumu yaliyopo katika mwongozo.
Dkt.Victorina anasema mkoa unaendelea kusimamia na kutekeleza mkataba wa lishe uliosainiwa na Mh Samia Suluhu Hassani wakati huo akiwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Tanzania na Mkoa uliingia makubaliano ya utekelezaji wa mkataba wa lishe na utekelezaji wa mkataba huo unafanyika mpaka katika ngazi ya kata,mtaa na vijiji.
Aidha anasema Mkoa hufanya vikao kwa ajili ya kutathimini mkataba huo kila baada ya miezi sita na tayari vikao vinne vimeshafanyika na hii imeongeza ari ya uwajibikaji katika kutekeleza Afua mbali mbali za lishe katika Mkoa.
Pia anasema mkataba huu wa lishe umeshashushwa mpaka ngazi ya kata na kijiji na tathimini ya mikataba hiyo hufanyika kila robo katika ngazi ya Halmashauri.
Kuhusu vipaumbele vya Mkoa,Dkt.Victorina anavitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za matibabu kwa watoto wenye utapiamlo mkali,kuimarisha huduma ya lishe kwa wajawazito,watoto wachanga,watoto wadogo,vijana balehe pamoja na wazee.
Mikakati mingine ni kuhamasisha matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa mfano chumvi yenye madini joto,mafuta na unga ulioongezwa virutubishi,kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yenye uhusiano na lishe,kuhamasisha ulimaji wa mazao yenye viini lishe kwa wingi,bustani za nyumbani na ufugaji wa wanyama wadogo na kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa za lishe kutoka ngazi ya kijiji mpaka mkoa.
Anasisitiza mganga mkuu huyo kuwa suala la lishe ni suala mtambuka na limepewa kipaumbele katika Mkoa wetu wa Singida na Mkoa utaendelea kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kutekeleza afua za lishe zenye kuleta matokeo chanya katika jamii.
Mganga mkuu huyo anasema bajeti ya kutekeleza shughuli za lishe katika Halmashauri za Mkoa wa Singida imeongezeka kutoka sh.i 115,697,932 kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 mpaka kufikia sh. 342,823,103 kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 sawa na shilingi 1,239 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano.
Anasisitiza pia kwamba Mkoa wa Singida utahakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kwa ajili ya kutekeleza shughuli za lishe kama zilivyopangwa na unaendelea kuhamasisha Halmashauri kutenga fedha za lishe kulingana na mwongozo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kutekeleza shughuli zilizopangwa.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake