November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Internews yawanoa waandishi wa habari,azaki ili kuimarisha uhusiano

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Jumla ya wadau wa habari 30 wa Mkoa wa Mwanza wakiwemo Waandishi wa Habari na Asasi za Kiraia(Azaki),wamejengewa uwezo wa kuimarisha uhusiano baina ya pande hizo mbili ili kuwa na maono ya pamoja ya kuwaletea maendeleo wananchi na waweze kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkazi nchini hapa wa shirika la Internews,Agnes Kayuni,wakati akifungua warsha hiyo ya siku mbili ilioanza Septemba 4 hadi 5, mwaka huu kwa wadau hao,inayofanyika jijini Mwanza iliondaliwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari wa Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (Ojadact) kwa ufadhili wa USAID kupitia mradi wa Boresha Habari.

Mkurugenzi Mkazi nchini hapa wa shirika la Internews,Agnes Kayuni

Kayuni ameeleza kuwa wamejikita kujengea uwezo jamii mbili za waandishi wa habari na Azaki kwa sababu ni sehemu inayotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi.

“Boresha Habari imejikita katika kujengea uwezo jamii hizi mbili,lengo kubwa ni kuwakutanisha ili kutafakari kwa pamoja je,uhusiano wa waandishi wa habari na azaki katika kazi zao zinaendaje? tunaridhika au kuna kuboresha zaidi,kutafakari,kuona jinsi gani tunaweza kujenga maono ya pamoja ili kuweza kuleta maendeleo na wananchi waweze kupata taarifa sahihi na kwa wakati,”ameeleza Kayuni.

Ameeleza kuwa lengo la warsha hiyo ni kuwakutanisha pande hizo mbili ili waweze kujenga uhusiano na kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi katika katika mambo mbalimbali ya kimkakati hiyo ni baada ya kubaini pengo lililopo kati ya waandishi wa habari na Azaki katika utendaji kazi wao.

“Tunategemea wakifanya kazi kwa pamoja wa kutetea agenda mbalimbali wataweza kuimarisha ili waweze kuleta mabadiliko ambayo yamekusudiwa mfano kuna azaki ambazo zimejikita kwenye elimu,haki za binadamu na mambo mengine,na waandishi kama wasimamizi wanaoleta sauti za wananchi,serikali na Azaki pamoja,hiyo ni nafasi ya kipekee kwaio ni muhimu hawa wawili waweze kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja,”ameeleza Kayuni na kuongeza kuwa

“Tumeona kuwa makundi hayo mawili yanahitaji mafunzo ili waweze kufanya kazi zao zaidi na ndio tumejikita hapo kwa upande wa Azaki tunatoa mafunzo ya wao kuweza kutumia vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,vyombo vya habari tunajaribu kuwasaidia ili wafanye kazi kwa weledi,wazingatie misingi iliopo ili wafanye kazi bila kupendelea upande wowote,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ojadact Edwin Soko, ameeleza kuwa lengo kuu ni kujenga uhusiano katika ya waandishi wa habari na Azaki kwamba pande zote ziweze kufanya kazi kwa pamoja wakati wote kwani wanajikita katika kuhakikisha wanaboresha maisha ya mwananchi.

“Tunataraji baada ya hapa Azaki na waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza na nchi kwa ujumla watajenga uhusiano ambao ni wa kudumu wa namna ya kufanya kazi kwa pamoja, Ojadact tunaishukuru Internews kwa kuweza kuwapika ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na ushirikiano,”ameeleza Soko.