Raphael Okello, Timesmajira Online,Musoma.
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC),imesema inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 199,501 kwa Mkoa wa Mara mwaka huu 2024, sawa na ongezeko la asilimia 17 ya wapiga kura waliopo kwenye daftari ya kudumu ya wapiga kura mkoani humo.
Baada ya zoezi hilo, Mkoa wa Mara unatarajiwa kuwa na wapiga kura zaidi ya milioni 1.3.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima,wakati akiwasilisha mada kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu ya wapiga kura kwa wadau wa uchaguzi mkoani Mara Agosti 25,2024 mjini Musoma.
Amesema uboreshwaji huo unaoendelea kwa awamu nchi nzima, utafanyika mkoani Mara, Simiyu na Manyara katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati ,Mji wa Babati, Hanang na Mbulu kuanzia Septemba 4-10, 2024 na kuwataka wanachi wajitokeze kujiandikisha na kurekebisha taarifa zao.
Pia amesema katika zoezi hilo nchi nzima, INEC inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwa sasa kwenye daftari baada ya uboreshwaji wa mwaka 2019/20.
Aidha jumla ya vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura vitatumika katika uboreshaji wa daftari hilo kwa mwaka 2024 ambapo vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Zanzibar.
Kailima ameongeza kuwa kuna ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika mwaka 2019/20.
Hata hivyo amesema kuwa,Tume hiyo inatarajia kuwa na jumla ya wapiga kura milioni 34,746,638 katika uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2025.Pia tume inatarajia jumla ya wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao wakati ambapo wapiga kura 594,494 wataondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwemo kwenye daftari hilo.
Awali akifungua mkutano huo wa wadau wa uchaguzi uliojumuisha viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanawake, vijana, walemavu, wazee wa kimila , vyombo vya dola na waandishi habari mkoani Mara, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwembegele,amewataka wadau hao kuhamasisha jamii kwenda kuboresha taarifa zao kwenye vituo.
Mwembegele amesema uboreshwaji huo kama ulivyo uboreshaji wa mwaka 2015 na 2020, utahusisha mfumo wa matumizi ya Biometeic Voters’ Registration (BVR) ambayo hutumika kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine.
Pia ametoa tahadhari kuwa asiwepo mtu ambaye atajiandikisha mara mbili kwa kuwa ni kosa la kisheria kufanya hivyo.
Taarifa zitakazoboreshwa ni pamoja na kurekebisha majina yaliyokosewa au kubadilisha jina au picha apendavyo mpiga kura,makazi kwa aliyehama, watakaokuwa wamefikisha umri wa kupiga kura ifikapo oktoba 2025, waliopoteza kadi au kadi kuharibika.
.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais