November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Imani za kushirikiana za sababisha wanawake kukimbiwa na waume zao

Na George Mwigulu,Timesmajira Online,Tanganyika.

Wanawake wengi waliokuwa wanaishi kwenye ndoa na waume za Kata za Ikola na Karema wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi wamekimbiwa na waume zao kwa hofu ya kukamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuunga mkono mtu anaye daiwa kuwa na uwezo wa kufichua wachawi maarufu kwa jina la Lambalaba au Kamchape.

Imetajwa kuwa wanawake hao kukimbiwa na waume zao kumeleta athari kubwa sio tu za kiuchumi bali wanalazimika kulea familia zao bila msaada wa waume zao huku wakibeba majukumu mapya ya kutoa majibu ya maswali ya watoto wao wanapoulizwa Baba ameenda wapi?.

Muonelano wa baadhi ya maeneo ya kijiji cha Karema ambako wanawake wamebaki peke yao baada ya waunaume kuwakimbia

Mmoja wa wanawake wa Kijiji cha Ikola jina tunalo amesema hayo leo katika Kijiji hicho kuwa kwa muda wa karibu wiki mbili sasa anaishi bila mwenza wake ambae amemkimbia bila hata ya kumuaga na kumwachia familia ya watoto watano huku akiwa hajui ni lini mume wake atarudi nyumbani

Amebainisha kuwa Kamchape/Lambalamba alipokuwa kwenye Kijiji hicho mume wake alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wanamuunga mkono afanye kazi ya kuwabaini wachawi lakini alivyoona watu waliokuwa wanamuunga mkono mganga huyo kuanza kukamatwa na Polisi nae pia alitokemea pasipo kujulikana na hakuna mawasiliano yoyote yaliyopo kati ya mume wake na familia.

Mama mwingine wa Kata ya Karema ambae hakuta jina lake litajwe kwenye Gazeti hili alisema mume wake amekimbia nyumbani kwa muda wa siku kumi sasa kwa kuhofia Kamata kamata inayoendelea ya watu walikuwa wakiumuunga mkono Kamchape na kufanya uhalifu wa mali mbali mbali za watu.

Ameeleza mume wake aliwaaga nyumbani siku kumi zilizopita kuwa anakwenda kwenye shughuli zake za kila siku za uvuvi katika Ziwa Tanganyika ambapo baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa msako mkali unaofanywa na jeshi la polisi wa kutafuta watu ambao waliunga mkono Imani za kichawi na kupora mali za watu alikimbia kusikojulikana.

Ameeleza kuwa walioathirika na kukumbiwa na waume zao ni wanawake wengi tu kwenye maeneo ya Kata ya Karema na pia wapo baadhi ya wanaume nao wamebaki bila wake zao kufatia wanawake kukimbia kukamatwa kwa kujihusisha na kumuunga mkono mganga huyo wa kienyeji .

Mkazi wa Kijiji cha Ikola Emanual Kibiriti alisema upatikana wa samaki katika maeneo ya Kata za Ikola na Karema umekuwa ni washida kutokana na wavuvi wengi ambao ndio walikuwa wakimuunga mkono Kamchape kukimbia na kuacha kufanya shughuli yao ya uvuvi.

‘’ Samaki wameadimika kwa sababu wavuvi wengi wamekimbia hawajulikani wako wapi? Ndugu mwandishi hali ya upatikanaji wa mboga ni mgumu sasa pia na kwa bahati mbaya anayepata shida hiyo ni mwanamke ambaye anajukumu kubwa la kuhudumia familia” Amesema Kibiriti.

Amefafanua kuwa idadi kubwa ya wanawake walikimbiwa na waume zao kutoroka kwa kuhofia kukamatwa na jeshi la polisi ni wake wa wavuvi wa samaki ingawa pia wapo na wanaume nao wamekimbiwa na wake zao na kuwaachia watoto.

Muonekano unaoonesha uharibifu wa mali za watu baada ya kufanywa na watu wanaounga mkono Kamchape.

Diwani wa Kata ya Ikola Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi Philemon Mollo anakili kuwa wanaume wengi wamekimbia familia zao kwa hofu ya kukamatwa na jeshi la polisi kwa sababu ya matendo ya kiharifu waliyoyafanya wakati wa zoezi ambalo lilifanywa na Lambalamba la kuumbua wachawi.

Mollo amebainisha kuwa jambo la kusitaabisha ni kwamba wanawake wengi nao walikuwa washirika wakubwa wa kumuunga mkono mtu huyo anayedhaniwa kuwa na uwezo wa kuwaumbua wachawi wakiamini kuwa utakuwa mwisho wa umasikini wao kwani wengi wao wanaamini chanzo cha umasikini ni uchawi unaofanywa na baadhi ya wananchi wenzao.

Kuhusu kupungua kwa wavuvi katika ziwa Tanganyika amedhibitisha ni kweli wamepungua kwa hofu ya kukamatwa na jeshi la polisi hususani wavuvi wengi ni raia wa nchi ya Burundi ambapo wengi wameingia kinyume na taratibu.

Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT wilaya ya Tanganyika,Mathew Andrew ameiomba jamii kuzingatia mafundisho ya Mungu kwa kuepuka kujihusisha na mambo ya Imani za kichawi ambayo yanaweza kuhatarisha maisha na mali zao.

Mchugaji huyo amebainisha kuwa nyakati tulizo nazo hivi sasa ni za mwisho kwani watu wengi watajitenga na mafundisho ya kweli ya Mungu na kufuata njia ambazo zitawafanya kukosa amani ambapo alitoa tahadhari kumrejea Mungu wao kwa faida ya maisha ya duniani na mbinguni pia.