December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Imani potofu dhidi ya wanawake katika uchimbaji madini kikwazo kufikia malengo

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online

Sekta ya uziduaji ikiwemo uchimbaji wa madini katika nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara imechangia na inaendelea kuchangia sehemu kubwa ya mauzo ya nje, mapato ya ndani ya kila mwaka kwenye mataifa ya Afrika.

Hata hivyo mwamko wa wanawake kujihusisha na shughuli za uchimbaji madini bado unakuwa na kuongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wanawake wachache walithubutu kujihusisha na uchimbaji huo.

Nchini Tanzania na maeneo mengine ya Afrika Mashariki wanawake wachimbaji wa madini wameanza kwa shughuli hizo, huku takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 27 tu ya wachimbaji madini wanawake wanahusika katika shughuli za uchimbaji wa madini.

Takwimu hizi zilizotolewa haziwakilishi shughuli nyingine zinazofanywa na wanawake kwa maendeleo na muendelezo wa sekta ya uchimbaji madini hata hivyo kwa sasa wanawake wengi wanamiliki migodi na wameajiri wanaume katika migodi yao.

Licha ya kuwepo kwa mwamko huo imeelezwa kuwa imani potofu dhidi ya wanawake katika masuala ya uchimbaji madini ni moja ya changamoto ambayo inarudisha nyuma jitihada za kundi hilo katika kujikomboa kiuchumi na kuchangia maendeleo kupitia sekta hiyo.

Hivyo muarobaini wa kutatua changamoto hiyo ni jamii kupewa elimu ili iweze kuachana na imani hizo potofu dhidi ya wanawake.

Na katika kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa zipo juhudi na jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika na zinafanyika ikiwemo iliofanywa na Shirika la Hakimadini chini ya ufadhili wa shirika la Womin African Alliance la Afrika Kusini kuandaa mafunzo kwa wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo wa madini Afrika kutoka nchi za Uganda,Kenya, Zimbabwe, Tanzania, Cameroon na Afrika Kusini.

Ambapo mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo na kisha kupeleka elimu kwa jamii wanazotoka ili ziwe na uelewa na kufahamu kuwa imani potofu dhidi ya wanawake katika sekta ya madini hazina ukweli na badala yake waachane nazo ili kufikia usawa wa kijinsia katika sekta hiyo.

Mkurugenzi wa Shirika la HakiMadini, Zawadi Joseph, akizungumza na timesmajira katika mafunzo ya siku nne yaliyofanyika jijini Mwanza, na kuratibiwa na shirika hilo,linalotekeleza kwa vitendo tamko la kimataifa la Haki ya Kusema Hapana ama Ndiyo (Right To Say No/ Yes) kwa ufadhili wa shirika la WoMin African Alliance la Afrika Kusini ambapo imeshirikisha
wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo wa madini Afrika kutoka nchi za Uganda,Kenya, Zimbabwe, Tanzania Cameroon na Afrika Kusini.

Ambapo Shirika la Hakimadini linafanya kazi katika maeneo ya machimbo na wanajikita zaidi kuangalia haki za wachimbaji wadogo na haki za jamii inayomzunguka na maeneo ya machimbo na wanapitia sera na sheria zinazolenga sekta husika ya madini na kuishawishi serikali kufanya marekebisho ya sheria ambayo tunaona ni kandamizi kwa jamii wanayofanya nayo kazi.

Zawadi anaeleza kuwa, wanawake wengi wanamiliki migodi na wameajiri wanaume ila sheria inatambua mwanaume zaidi kwa sababu ya uhalisia wa sekta hivyo na wengi wanaozama migodini kuchimba madini ni wanaume.

Anaeleza kuwa bado sekta hiyo ni kandamizi kama walivyo sikia kutoka kwenye mafunzo kutokana na imani potofu kuwa mwanamke anaposogelea kwenye mgodi akiwa katika siku zake za hedhi basi madini yanapotea hali ambayo siyo kweli kwani hakuna uhusiano kati ya kukosekana kwa madini na mwanamke kuwa katika siku zake.

Hivyo aneeleza kuwa jamii inatakiwa ipewe elimu na itambue kuwa hizo ni imani potofu tu wala siyo kweli kwamba mtu akilala na mwanamke mzee basi atapata madini mengi au mwanamke akiwa katika siku zake za hedhi basi madini yanapotea.

Pia anaeleza kama mashirika wanahitaji kutoa elimu kwa jamii hasa jamii husika inayolenga sekta ya madini kuwaelimisha kuwa hizo ni imani potofu na zitazidi kuwarudisha nyuma wao wanawake na hawataweza kwenda mbele.

“Tunakazi kubwa mbele yetu ya kuelimisha jamii tusiamini zaidi mila potofu tukitaka kusonga mbele zaidi hasa tukitaka kuwainua wanawake kiuchumi na tusiwe tegemezi kwa kina baba,serikali na jamii,elimu tunayoipata hapa kwenye mafunzo haya isiishie hapa bali tuipeleke katika maeneo yetu kwa watu ambao hawana uelewa ili wasizidi kuamini imani potofu,”anaeleza Zawadi na kuongeza kuwa

“HakiMadini imekuwa ikitoa elimu katika jamii kuondokana na dhana hiyo na katika maeneo ambayo tumefika na kutoa elimu, wanawake wameanza kushiriki kwenye uchimbaji madini na wamewaajri wanaume kwenye migodi yao,”.

Pia anaeleza kuwa serikali iendelee kutambua mchango wa wanawake hasa katika sekta ya madini na sheria isimamie kile ilicho tamka wanawake wataanza kujikita kwenye shughuli husika za uchimbaji madini bila hofu wala kuogopa.

Mkurugenzi wa taasisi ya Africa Transcribe, Evans Rubara,anaeleza kuwa kuna sheria nyingi zimeundwa katika nchi za Afrika kusini,Zimbabwe,Kenya na Uganda pamoja na sheria hizo zinahitaji makampuni ya uchimbaji kuwezesha wananchi na wanaweza kufaidika na shughuli za uchimbaji mdogo au mkubwa katika maeneo yao.

Rubara anaeleza kuwa katika Bara la Afrika moja ya vizingiti vilivyopo kwa wachimbaji wanawake ni kutokushirikishwa katika uchimbaji kutokana na mila potofu zilizopo ambazo zimekuwa zinadhofisha juhudi za wanawake katika kujihusisha na uchimbaji huku asilimia 27 ya wanawake ndio wanaojishughulisha kwenye sekta hiyo.

Mwakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini ya Rubby kutoka Mundala mkoani Arusha Rose Olokwani, anaeleza kuwa kwa muda mrefu wanawake waliwekwa kando kushiriki kwenye shughuli za madini kutokana na mfumo dume.

Lakini kutokana na jitihada za shirika la HakiMadini kuelimisha wananchi, utamaduni huo umeanza kutoweka na sasa wanawake wameanza kujikita kwenye uchimbaji madini na kujikwamua kiuchumi.

Mchimbaji madini ya dhahabu katika machimbo ya Mugusu mkoani Geita Benadetha Petro,anaeleza kuwa mkutano huo ni muhimu kwa kuwa umekutanisha wanaharakati kutoka mashirika mbalimbali ya Afrika na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu namna sekta za uwekezaji zinaendeshwa katika mataifa yao hususani kuwasaidia wanawake kunufaika kiuchumi na raslimali zilizopo katika maeneo yao.

Mratibu wa shirika la Center for Natural Resources Governance kutoka nchini Zimbabwe Zinzile Fengu,anaeleza kuwa nchini kwao wanaamini kuwa ukilala na mwanamke mzee unapata dhahabu nyingi huku Raya Ahmed kutoka nchini Kenya ameeleza kuwa jadi na mila zimekuwa zinawakandamuza wanawake kimaendeleo.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka shirika la WoMin African Alliance nchini Cameroon, Georgine Kengne alitahadharisha kuwa baadhi ya miradi imekuwa na madhara kwa wananchi ikiwemo uharibifu wa mazingira hivyo ni vyema wananchi kushirikishwa na kutoa maamuzi hatua itakayosaidia kujiepusha na madhara hayo.

Kengne aneleza kuwa baada ya kongamano la mada za kijamii la uchumi wa uziduaji huko Johannesburg mwaka wa 2018, TSF-Mining na uchumi wa uziduaji walifanya misururu ya mitandao ili kupata muafaka kwa kuzingatia tofauti za uelewa wa “haki ya kusema hapana”

Anaeleza kuwa mikakati mahususi yenye viwango tofauti vya uamuzi na mafanikio yanafanyika duniani kote ni muhimu kuangazia wanawake wanaoongoza mapambano ya kusema hapana kwa uchimbaji madini haribifu.

Wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo kutoka nchi za Uganda, Kenya, Zimbabwe, Tanzania, Cameroon na Afrika Kusini,wakiawa katika mafunzo ya siku ya kujengewa uwezo yaliyoratibiwa na shirika la Hakimadini kupitia ufadhili wa shirika la Womin African Alliance la Afrika Kusini,wakiwa katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza kwa muda wa siku nne.(picha na Judith Ferdinand)
Mkurugenzi wa Shirika la HakiMadini, Zawadi Joseph kushoto akizungumza katika mafunzo ya siku yanayofanyika jijini Mwanza na kuratibiwa na shirika hilo,linalotekeleza kwa vitendo tamko la kimataifa la Haki ya kusema hapana ama ndiyo(Rights to say No/yes) kwa ufadhili wa shirika la Womin African Alliance la Afrika Kusini ambapo imeshirikisha wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo wa madini Afrika kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Zimbabwe, Cameroon na Afrika Kusini.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkurugenzi wa taasisi ya Africa Transcribe, Evans Rubara (akiongoza majadiliano katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Zimbabwe, Cameroon na Afrika Kusini ambayo yanafanyika jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Mwakilishi kutoka shirika la WoMin African Alliance nchini Cameroon, Georgine Kengne akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za wananchi na wachimbaji wadogo kutoka nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Zimbabwe, Cameroon na Afrika Kusini ambayo yanafanyika jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)