December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yaunga mkono jitihada za Serikali kwa kupanda miti 500

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

WILAYA ya Ilemela imeunga mkono kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu isemayo ‘Tunza mazingira ,okoa vyanzo vya maji kwa usatwi wa viumbe hai kwa uchumi wa Taifa’ kwa kupanda miti 500 ikiongozwa na Mkimbiza Mwenge Kitaifa Abdalla Shaib Kaim.

Ambapo mbali na upandaji miti pia alikagua mradi wa kudhibiti taka ngumu na kugawa vifaa vya kufanyiwa usafi kwa viongozi wa soko la Kiloleli Kata ya Ibungiro lengo ikiwa ni kudhibiti uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

.Miti hiyo imepandwa katika shule ya sekondari ya Wavulana ya Bwiru iliopo Kata ya Pasiansi wilayani Ilemela wakati Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa alipotembelea shuleni hapo kwa ajili ya kukagua shughuli za mazingira na club ya wapinga rushwa.

Kaim akizungumza na wananchi,wanafunzi na viongozi mbalimbali mara baada ya kushiriki zoezi la upandaji miti shuleni hapo ameipongeza Wilaya ya Ilemela kwa kupanda miti mingi.

Ambapo kitendo hicho ni ishara ya kuwa Ilemela inaunga mkono kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu na jitihada za serikali za kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mbali na hayo pia amewahimiza viongozi wa soko la Kiloleli kuendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea za utunzaji wa mazingira kwa kuhamasisha utunzaji na usafi wa mazingira kuepuka utupaji wa taka ovyo pamoja na mifuko ya plastki.

Awali Perpetua Moyo,akisoma taarifa ya shughuli ya upandaji miti kwa kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,amesema kuwa Wilaya ya Ilemela inatekeleza shughuli za uhifadhi na utunzaji mazingira kwa kutumia mpango mkakati ulioandaliwa kwa kuzingatia mpango wa muda mrefu na muda mfupi kwa kushirikiana na taasisi za umma, binafsi na wadau mbalimbali wa mazingira.

“Lengo ni kuhifadhi mazingira kwa njia ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda vyanzo vya maji,kupanda miti ya matunda, mbao na kivuli katika maeneo ya taasisi hususani shule za msingi, sekondari, zahanati, vituo vya afya na hospitali,kujenga uwezo wa kitaalamu kwa jamii katika kutunza, kulinda na kuhifadhi rasilimali za miti kwa njia endelevu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kulinda bionowai,”amesema Moyo.

Moyo amesema kuwa uhifadhi wa mazingira una faida kuu tatu ikiwemo za kimazingira, kiuchumi na kijamii ambapo misitu husaidia kupatikana kwa mvua na kutunza vyanzo vya maji, huifanya ardhi ishikamane na hivyo kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Pia husaidia kukinga upepo na hivyo huepusha athari zaidi za upepo mkali,utoaji malighafi mbalimbali kama vile magogo kwa ajili yakutengeneza karatasi na vifaa vya ujenzi,utoa hewa safi ya oxygen na hutoa madawa yanayotumika kutibu magonjwa mbalimbali.

Kwa upande wake Peter Yohana akisoma taarifa ya mradi wa huduma ya udhibiti wa taka ngumu na usafi wa mazingira kwa wananchi kwa Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, ameeleza kuwa Wilaya ya Ilemela inakadiriwa kuzalisha wastani wa tani 679 za taka ngumu kwa siku.

Ambapo tani 432 zinazalishwa kwenye kata 13 zenye sura ya mjini na tani 247 kwenye kata 6 zenye sura ya kijiji huku ikisafirisha wastani wa tani 344.4 ya taka ngumu kwa siku zinazozalishwa mjini na inatumia wastani wa tani 53 ya taka kama malighafi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa kama mkaa mbadala, chakula cha mifugo, bomba za maji na mifuko ya nafaka.

“Mradi huu una gharama ya zaidi ya milioni 33 ambapo ujenzi wa uzio na skip pads zaidi ya milioni 3,mabirika ya taka ngumu (skip buckets 2) zaidi ya milioni 27 na vifaa vya usafi zaidi ya milioni 3 huku mkakati ni kununua makasha ya kuhifadhi taka ngumu,kununua magari ya usafirishaji wa taka ngumu pamoja na kuendelea kuhamasisha jamii katika kufanya usafi na kutunza mazingira yanayowazunguka bila shuruti,”amesema.