November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yatoa lishe kwa watoto 40 wenye utapia mlo

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imetumia kiasi cha milioni 7.45 kununua chakula lishe ambacho kimetolewa kwa watoto 40 wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miaka 5 wenye utapiamlo mkali huku lengo likiwa ni kuwafikia watoto 100 kwa kila robo ya mwaka.

Ikiwa ni jitihada za kutokomeza utapiamlo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambapo kupitia kitengo cha lishe imeanzisha zoezi la ugawaji wa chakula lishe kwa watoto wenye utapiamlo mkali katika mitaa yote 171 ya halmashauri hiyo.

Ambapo zoezi la ugawaji wa chakula lishe kwa watoto wanaoishi katika Halmashauri hiyo lililongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi lililofanyika Kituo cha Afya cha Buswelu,wilayani humo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Hassan Masala.

Akikabidhi chakula hicho kwa wazazi wa watoto hao Mariam amesema kuwa halmashauri hiyo Ilemela inaunga mkono juhudi za serikali za uboreshaji wa huduma za lishe kwa kutoa fedha katika sekta hiyo kwa kutambua umuhimu wa wananchi wote kuwa na lishe bora tangu wakiwa wadogo ili kuwa na nguvu kazi imara katika ujenzi wa taifa.

Sanjari na hayo amewapongeza wakina baba waliofika kituo cha afya Buswelu kwa ajili ya kupata huduma za kliniki pamoja na kusikiliza elimu ya lishe huku akiwasihi wanaume waliopo nyumbani kuhamasika na kutenga muda wa kuwa na watoto wao.

” Nawapongeza kina baba waliojitokeza hapa leo kuleta watoto wao kupata huduma za kliniki pia kusikiliza elimu ya lishe inayotolewa na wataalam ni kitu kizuri na kinajenga upendo wa mtoto kwa wazazi wote wawili baba na mama,”ameeleza Mariam.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Nyabwire Lukumai amesema kuwa halmashauri hiyo kupitia idara ya afya inaendelea kuhamasisha ushiriki wa kina baba katika huduma mbalimbali za uzazi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka watoto wao kliniki.

” Mtoto ni wa wote hivyo kwa pamoja baba na mama wanawajibika katika malezi na nyanja zote,”mesema Nyabwire.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe ya Halmashauri hiyo Pili Kassim amesema halmashauri imeendelea kutenga kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka 5 katika kuhakikisha watoto wote wanafikiwa kwa lengo la kupunguza na kutokomeza utapiamlo na kuendelea kuhamasisha jamii kulima mazao yenye viini lishe kwa wingi ili kuimarisha afya zao.

Wakazi wa Kata ya Kahama mtaa wa Buyombe wameipongeza serikali kwa kuanzisha utaratibu wa ugawaji lishe sambamaba na utoaji wa elimu endelevu ya lishe kwa wananchi.

Nae Juma Alphonce mkazi wa Kata ya Shibula anajivunia kuwa baba bora kwa kutoa huduma mbalimbali zinazohitajika kwa mwanae.