March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yapitisha mpango na  bajeti ya bilioni 101.74 mwaka 2026/2027

*Msisitizo ukiwekwa ukusanyaji wa mapato kwa njia rafiki kwa wananchi na wafanyabiashara

*Madiwani watakiwa kushirikiana na wataalamu kukusanya mapato

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Madiwani la Halmashauri  ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wamepitisha mapendekezo  ya mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027  wa bilioni 101.74 huku msisitizo ukiwekwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wananchi.

Akizungumza katika Baraza la Madiwani la kupokea na kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027,lililofanyika Januari  26,2026,Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Herbert Bilia,amesema bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 imezingatia vipaumbele vya kata zote 19 za manispaa hiyo.

Huku ikijikita katika dira ya maendeleo ya 2025-2050 inayolenga kuboresha huduma za jamii na miundombinu,ambapo amesema halmashauri hiyo  itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo licha ya changamoto ya upungufu wa rasilimali katika baadhi ya maeneo, hususani miundombinu,afya na elimu.

Bilia amesema,mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri inakadiria kukusanya  na kutumia kiasi cha bilioni 16.45 mapato ya ndani kati ya fedha hizo bilioni 7.24 zitaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Sarah Ng’hwani,amewasisitiza wanao kusanya mapato watumie njia rafiki na wasitumie nguvu.

Hivyo amewataka watumie njia ya kuwahamasisha,kuwaelimisha wafanyabiashara na kujenga nao urafiki ili waweze kukusanya mapato kwa amani  kwani wanataka kuona wananchi wanapata tabasamu.

“Tuunganishe nguvu katika jambo hili la ukusanyaji wa mapato,tunaponunua vitu hata sisi viongozi  tunapaswa kudai risiti, kwani tunapo dai risiti moja kwa moja unakuwa umelipa kodi,”amesema Sarah.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Dkt.Maria Kapinga,amewaomba Madiwani hao kutoa ushirikiano wakati wa kukusanya mapato pamoja na elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi na kukusanya mapato.

Mjumbe wa wa Kamati ya Huduma,Diwani wa Kata ya Nyasaka,Fredy Kisaka,amesema wananchi wanahitaji maendeleo hivyo ili kukafanikisha jambo hilo amewaomba Madiwani  kuhakikisha wanabuni vyanzo vipya vya mapato katika Kata zao.

“Pia ili tutekeleza haya yote yalio mbele yetu,Madiwani tushirikiane kwa pamoja na wataalamu pamoja na kuhakikisha tunabana matumizi,”amesema Kisaka.

Diwani wa Kata ya Kitangiri Donald Ndaro,amesema watafute fedha katika vyanzo rafiki  ili kuimarisha  vyanzo vya mapato vya ndani huku akiwataka Madiwani wenzake kuhakikisha wanashirikiana na wataalamu katika kukusanya mapato.

Pia ameomba Halmashauri  hiyo,kukamilisha miradi viporo na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo endelevu.

Naye Diwani Viti maalumu Sara Manyama,amesema,”Tukatoe elimu kwenye maeneo yetu kwa wananchi katika kukusanya mapato ili tuweze kuleta maendeleo,kwani bajeti hiyo imezingatia maeneo yote muhimu ya maendeleo na itawezesha kuimarisha ustawi wa wananchi pamoja na kuboresha miundombinu yetu endapo itatekelezwa ipasavyo,”.

Diwani wa Kata ya Nyamh’ongolo Safia Mkama,amesema wanaimani kuwa bajeti hiyo itaenda kuongeza maendeleo katika Kata zao na kuboresha barabara pia  huku akimpongeza Mchumi kuweka usawa wa bajeti kwa kila Kata.

Diwani wa Kata ya Nyakato, Jonathan Mkumba,amesema,”Tushirikiane katika kutekeleza  bajeti hii ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na kuongeza jitihada katika kukusanya mapato,”.