January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yakusanya asilimia 68 makisio ya bajeti 2023/2024

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Hadi kufikia Machi 31, mwaka huu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 10.1 sawa na asilimia 68 ya maksio ya bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha wa 2023/24.

Huku katika kipindi cha robo ya tatu halmashauri hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi yenye jumla ya zaidi ya bilioni 3.9 kutoka Serikali Kuu ikiwemo ya TASAF na TACTIC.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Marco Isack katika mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kipindi cha robo ya tatu Januari hadi Machi mwaka wa fedha wa 2023/24 kilichofanyika Mei 11,2024 kwenye halmashauri hiyo.

“Katika kipindi cha robo ya tatu halmashauri imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia TASAF yenye jumla ya zaidi ya milioni 376 kati ya hizo zaidi ya milioni 196.6 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana 80 shule ya sekondari Kayenze huku zaidi ya milioni 179 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana 80 wa shule ya msingi Buswelu,” ameeleza Isack na kuongeza kuwa

“Halmashauri kupitiaTACTIC imeendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Buswelu-Busenga-Cocacola Km 3.3 na barabara ya Buswelu –Nyamadoke-Nyamh’ongolo Km 9.5 ambapo tayari Mkandarasi amelipwa zaidi ya bilioni 3.5 na mradi umefikia asilimia 12 ya utekelezaji,”.

Akizungumzia suala la mapato ya ndani Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa katika robo ya tatu zaidi ya milioni 679.3 zilielekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata za halmashauri hiyo ikiwemo milioni 170 kwa ajili ya malipo ya Mkandarasi wa barabara ya lami kutoka hospitali ya Wilaya ya Ilemela kuelekea Ilalila Km 13.

Zaidi ya milioni 167 kwa ajili ya mchango wa fedha katika mfuko wa Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu asilimi 10,zaidi ya milioni 164 kwa ajili ya ulipaji fidia maeneo mbalimbali ikiwemo Buswelu –Nyamadoke-Nyamh’ongolo,Buswelu-Busenga-Cocacola zaidi ya milioni 12.5 kwa wananchi 4.

Huku maeneo mengine ni Mitaa ya Nyafula, Sangabuye na Lugeye zaidi ya milioni 16.3 kwa wananchi 5,eneo la viwanda Nyamh’ongolo milioni 4 kwa wananchi 2.

Eneo la shule ya sekondari Nyamanoro zaidi ya milioni 25 kwa mwananchi mmoja,shule ya sekondari Lumala na shule ya msingi Mwambani milioni 48.02 kwa wananchi wawili,Ibinza Nyamh’ongolo zaidi ya milioni 2.8 kwa mwananchi mmoja,Shibula milioni 2 kwa mwananchi mmoja,Pasiansi milioni 3 kwa mwananchi mmoja pamoja na eneo la East Buswelu zaidi ya milioni 49.9 kwa wananchi 4.

Aidha zaidi ya milioni 41.1 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo na mabafu 3,katika mialo ya Mihama,Igombe,Kabangaja pamoja na ujenzi wa ofisi ya Mwalo wa Mihama huku zaidi ya milioni 34 kwa ajili ya kununulia mashine za POS 50 kwa ajili ya kukusanyia mapato.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga amesisitiza Madiwani katika maeneo yao wasimamie ukusanyaji wa mapato ili fedha zitakazopatikana ziweze kumaliza maeneo ambayo bado hawajakamilisha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Nao baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Nyakato Jonathan Mkumba amewaomba wataalamu wa Ardhi kuanzisha kliniki ya ardhi kwa kila Kata ili kusuluhisha na kutatua migogoro ya ardhi kwani imekuwa kero katika maeneo yao.